NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa (JWT), Hamis Livembe, amesema mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania uliomalizika hivi karibuni ulikuwa wa haki, halali na uliozingatia taratibu zote, huku akikanusha madai ya kuwekwa kwa viongozi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 19,2025 jijini Dar es Salaam, Livembe amesema hakuna ukweli wowote katika madai yanayosambaa kuwa viongozi wa jumuiya hiyo waliwekwa, akieleza kuwa yeye mwenyewe amewahi kuwa madarakani miaka minne iliyopita bila mabadiliko yoyote ya misingi ya uendeshaji wa jumuiya.
Katika hatua nyingine, Livembe amesema JWT imeitaka Serikali pamoja na Tume ya Maboresho ya Sheria za Kodi kutoa hadharani matokeo ya kazi iliyofanywa na Tume hiyo, akieleza kuwa wafanyabiashara wana hamu kubwa ya kujua mapendekezo yaliyotolewa, hasa baada ya uchaguzi kumalizika.
Amesema tume hiyo iliundwa kwa lengo la kufanya maboresho ya sheria za kodi lakini iliongezewa muda wa utekelezaji wa majukumu yake kutokana na masuala ya uchaguzi, hivyo kwa sasa ni wakati muafaka kwa tume kurejea rasmi kazini na kuwasilisha mapendekezo yake, ikiwemo yale yanayohusu kupunguza mzigo wa kodi na kuzijumlisha kodi mbalimbali katika kapu moja.
Akizungumzia hali ya biashara wakati na baada ya uchaguzi, Livembe amesema licha ya kuwepo kwa vurugu zilizowafanya baadhi ya wateja kukimbia maeneo ya biashara, tathmini ya JWT katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya imeonyesha kuwa hali ya biashara imerejea katika hali ya kawaida na mazingira ya usalama yametengemaa.



