NA ASHRACK MIRAJI,LUSHOTO,TANGA
MAANDALIZI ya tukio la Magamba Forest Walkathon and Adventure Season III yamekamilika kwa asilimia 85 huku waandaaji wakieleza kuwa kila kitu kinaendelea vizuri kuelekea kilele chake.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 17 hadi 20 Desemba mwaka huu katika Manispaa ya Lushoto, mkoani Tanga.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Misitu ya Mazingira Asilia Magamba, Christoganus Vyokuta, amesema kuwa kuanzia Desemba 17 hadi 19 mwaka huu, wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii watapata fursa ya kujitangaza na kuonesha huduma na bidhaa zao mjini Lushoto.
Vyokuta amesema kuwa kilele cha tukio hilo kitafanyika Desemba 20,2025 ambapo washiriki watahusika katika matembezi maalumu ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Magamba, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani na uhifadhi wa mazingira.
Ameeleza kuwa lengo kuu la Magamba Forest Walkathon and Adventure Season III ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika suala zima la uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii ikolojia, hususan kwa kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini.
Mhifadhi huyo amewataka wananchi na wadau wa sekta ya utalii kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kulinda rasilimali za asili na kuhakikisha uhifadhi endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

