NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa mikopo ya Elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh.Bilioni 464 mwaka 2021 hadi kufikia Sh.Bilioni 916.7 mwaka 2025/26 na kwamba katika mikopo hiyo itatolewa pia kwa wanafunzi wa vyuo vya Kati.
Profesa Mkenda ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na Waandishi wa Habari ambapo amesema mikopo hiyo sasa rasmi kutolewa kwa vyuo vya kati huku akisisitiza kuwa hiyo ni fursa kubwa imeongezwa kwa vijana.
Hata hivyo amesema vijana watakaochukuliwa na serikali kisha kupelekwa kusoma katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ajili ya kupata ujuzi wa kujiajili au kuajiriwa watatakiwa kutoa kiasi cha Sh. 120,000 kwa kukaa bweni na kutwa ni sh. 60,000.
“Pia karibia tunakamilisha ujenzi kampasi za vyuo vikuu vya Serikali katika mikoa ambayo ilikuwa haina kabisa kampasi ya vyuo hivyo, tutaanza na Kagera na Lindi mikoa hii ilikuwa haina kampasi yoyote ya vyuo vikuu, kwa ujumla wake bajeti sekta mzima ya Elimu chini ya serikali ya awamu ya sita
Profesa Mkenda amefafanua kuwa
Serikali imeanzisha mfumo wa mikondo miwili katika elimu ya sekondari ili kuwapa wanafunzi uchaguzi unaoendana na uwezo na malengo yao ya baadaye.
Amesema mwanafunzi atachagua mkondo anaoutaka baada ya shule ya msingi kwa
ushauri wa wazazi na walimu na kusisitiza kuwa mikondo hiyo ni mkondo wa elimu ya jumla, unaojikita katika masomo ya nadharia na kitaaluma pia kuna mkondo wa elimu ya amali, unaolenga ujuzi wa vitendo, utendaji na maandalizi ya kazi.
“Serikali pia imeweka mfumo unaomruhusu mwanafunzi kubadili mkondo, ambapo mwanafunzi wa elimu ya amali akihitimu kidato cha nne anaweza kuendelea na Kidato cha tano na sita katika mkondo wa elimu ya jumla endapo atapenda. Wahitimu wa mkondo wa amali watapatiwa vyeti vinavyotambuliwa kitaifa kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA))
“Hakika vitu hivi vitakavyowasaidia kuajiriwa,
kujiajiri au kuanzisha biashara. Tunafanya haya yote lengo ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa fursa kwa kuchagua elimu ya amali, kwani mikondo yote miwili inathaminiwa sawa katika kujenga rasilimali watu nchini,” amesema
Hata hivyo Profesa Mkenda amesema Serikali inajiandaa kuanza utekelezaji wa mageuzi makubwa ya mfumo wa elimu yatakayobadilisha muundo uliodumu kwa zaidi ya nusu karne.
Amesema chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali inakuja na mfumo mpya wa 6+4+2/3+3+, ambao utaifanya elimu ya msingi kuwa miaka sita badala ya saba.Mfumo huo pia utaanzisha elimu ya lazima ya miaka 10, tofauti na mfumo wa sasa wenye miaka saba.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, utekelezaji wa mwanzo umeanza kupitia mitaala mipya kwa wanafunzi wa darasa la tatu ambao ifikapo mwaka 2027 watakuwa wa kwanza kufikia darasa la sita na kufanya mtihani wa kupima uwezo kabla ya kuendelea moja kwa moja na elimu ya sekondari ya kati hadi kidato cha nne.
Utekelezaji rasmi wa mfumo mpya kitaifa unatarajiwa kuanza mwaka 2028.
Aidha , Profesa Mkenda, amesema Serikali imeweka vivutio maalumu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kupitia mpango wa Samia Scholarship, akisisitiza kuwa sayansi ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesema mpango huo umeongezewa wigo kupitia Samia Scholarship Extended kwa baadhi ya fani za shahada ya uzamili, hususan maeneo yenye uhitaji wa kitaifa kama sayansi ya nyuklia, ili kuzalisha wataalamu watakaotumia vyema rasilimali za nchi.
Profesa Mkenda ameongeza kuwa eneo la akili unde limepewa kipaumbele kutokana na mchango wake katika usalama wa taifa, uchumi, benki, kilimo na maendeleo ya teknolojia, hivyo Serikali imeamua kuwapeleka wanafunzi bora zaidi kusoma nje
ya nchi.
Ameeleza kuwa tayari vijana 50 wamechaguliwa na wapo kwenye mafunzo ya maandalizi katika Taasisi ya Nelson Mandela African Institute of Science and Technology (NM-AIST) Arusha, kabla ya kusafiri kwenda Johannesburg, Afrika Kusini, kama kundi la kwanza mwishoni mwa Januari.




