NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WANAWAKE wameshauriwa kutokukata tamaa badala yake wajitume, wawe na umoja, wasaidiane na kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii kwa lengo la kujiimalisha kiuchumi ili kuondokana na utegemezi pamoja na umaskini.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Brave Women, Irene Mapendo wakati wa kongamano la wanawake lililoandaliwa na taasisi hiyo na kuwaleta pamoja wanawake mbalimbali wajasiriamali.
Amesema katika dunia ya sasa ambako nafasi ya mwanamke katika uchumi inaendelea kuimarika, kikundi cha Brave Women kimekuwa mfano halisi wa nguvu, uthubutu na umoja kwa kuwaleta pamoja wanawake na kujifunza fursa mablimbali zilizopo.
Mapendo amesema kikundi hicho, ambacho kinawakutanisha wanawake wa rika na taaluma mbalimbali, kimeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafunzo, ujasiri na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake nchini.
“Mimi natambua kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao na jamii, endapo wataamua kusimama imara, kusaidiana na kutokata tamaa hata hivyo kupitia Brave Women, wanawake wengi upata fursa ya kujifunza vitu mbalimbali hasa za kusaidiana, masuala ya uchumi, ujasiriamali na usimamizi wa fedha maarifa ambayo yanawainua na kuwapa uelewa mpana katika kupanga mustakabali wao,” amesema Mapendo na kuongeza
“Hatutaki mwanamke abakie nyuma, tumejenga kikundi kitakachowafungulia wanawake milango ya maarifa na kuleta mabadiliko chanya. Lakini zaidi ya hapo, tumeendelea kutoa msaada kwa watoto na makundi ya wahitaji ili kurudisha kwa jamii sehemu ya kile tunachokipata. Huo ndiyo moyo wa Brave Women.”
Naye Makamu Mwenyekiti wa Brave Women, Bumi Mwampeta anasisitiza kuwa wanawake ni jeshi kubwa, na ni muhimu kulitambua hilo mapema ili kuhakikisha unapambana katika kujikwamua na umasikini.
Hata hivyo Mwampeta amewataka wanawake kuepuka kuyumbishwa na mahusiano kiasi cha kuathiri afya ya akili. “Mapenzi ni sehemu ya maisha,” asema Bumi, “lakini yasitufanye tupunguze thamani yetu au tukose mwelekeo. Mwanamke mwenye nguvu ni yule anayejitambua na kufanyakazi kwa bidii.”
Kwa upande mwingine, mwanachama wa kikundi hicho ambaye pia ni mhasibu, Dorice Meena ametoa mwaliko kwa wanawake wengine kujiunga na Brave Women ili kufungua milango ya fursa.
Ameeleza kuwa kupitia kikundi hicho, wanawake wamekuwa wakijiona sio tu kama washiriki wa mafunzo ya kiuchumi, bali pia kama familia inayoshirikiana na kusaidiana. “Tunajifunza, tunajikwamua, tunapata marafiki wapya na mitazamo mipya,” anasema Meena
Naye mwanachama mwingine, Elizabeth Mpenzu amesema anahimiza wanawake kuacha tabia ya kujifungia majumbani na badala yake washiriki shughuli mbalimbali za kijamii.
Anaeleza kuwa mwanamke anapotoka nje na kushiriki matukio mbalimbali, ndipo huona fursa mpya, kujifunza biashara zinazochipukia na kuelewa mitazamo ya watu wengine. “Huwezi kujua dunia inafanya nini kama bado upo ndani,” amesema Mpenzu
Brave Women imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuamsha uwezo wa mwanamke, kumjengea ujasiri na kumpa ramani ya kujiendeleza. Kikundi hiki kinathibitisha kuwa pale wanawake wanapoungana, mafanikio yao huwa ni makubwa kuliko changamoto wanazokutana nazo.




