NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema inatambua mchango wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika kupanua huduma jumuishi za kifedha, hususan kwa wanawake, vijana na wajasiriamali wadogo na wa kati, kupitia ubunifu wa hatifungani ya Stawi Bond.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, katika hafla ya kutangaza matokeo ya kuorodheshwa kwa dhamana hiyo chini ya TCB.
Mwandumbya amebainisha kuwa Serikali inatambua historia ya zaidi ya miaka 100 ya TCB katika kuhudumia Watanzania, na kuipongeza benki hiyo kwa kuzindua Stawi Bond kama mchango muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21–2029/30.
Mwandumbya, ameongeza kuwa Stawi Bond imewezesha upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu ambao utaongeza uwezo wa TCB kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali na kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi.
“Nawapongeza TCB kwa kupata idhini ya CMSA, hatua inayoongeza uhakika kwa wawekezaji na kuimarisha imani katika mifumo ya kifedha nchini,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo, amesema kuwa ukusanyaji wa Shilingi bilioni 140.24 sawa na mara tatu ya lengo la awali lunaonyesha imani kubwa ya wananchi katika dira ya benki hiyo na dhamira ya kukuza uchumi jumuishi.
Mihayo ameongeza kuwa Stawi Bond imevutia kwa kiwango kikubwa wawekezaji wadogo na wa kati, tofauti na hatifungani nyingi zinazotawaliwa na wawekezaji wa taasisi, jambo linalodhihirisha kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika masoko ya mitaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, amebainisha kuwa mafanikio ya Stawi Bond yanaakisi ukuaji endelevu wa masoko ya mitaji nchini na kufungua fursa kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kutumia masoko hayo kupata fedha kwa ajili ya biashara na miradi ya maendeleo.






