NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kuhakikisha huduma za mawasiliano nchini zinakuwa imara, za uhakika na kwa gharama nafuu limezindua huduma mpya ya T. Fibre Triple Hub Internet au Faiba Tripo Hub yenye lengo la kufikisha huduma za kisasa za Intaneti hadi kwenye makazi ya watu, ofisi na sehemu za biashara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma hiyo, Meneja Promosheni wa TTCL, Janeth Maeda amesema shirika hilo limeendelea kusikiliza kwa makini maoni, mahitaji, na matarajio ya Watanzania kutoka kila pembe ya nchi.
Maeda, amesema kutokana na kusikiliza huko maoni wamekuja na huduma hiyo mpya ambayo inaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya TTCL ya kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa Watanzania.
“Tumejifunza kwamba, wananchi wanahitaji huduma rahisi kutumia, za gharama nafuu, lakini zenye ubora wa juu itakayotoa tafsiri ya thamani halisi kwa fedha wanazotumia katika hurakati za kuboresha maisha yao,” amesema
Amesema dunia kwa sasa inaendeshwa kwa nguvu za teknolojia na mawasiliano, hivyo huduma ya intaneti ya kasi siyo tena anasa bali ni hitaji muhimu katika maisha ya kila siku ya wananchi nyumbani, shuleni, ofisini na kwenye biashara.
Aidha, Maeda amebainisha kuwa TTCL imewekeza kikamilifu katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa urahisi, ubora wa juu na kwa gharama nafuu, ili kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali wanapoishi au wanapofanya kazi.
Amesema huduma hiyo mpya ya Faiba Tipo Hub imebuniwa mahsusi kwa kizazi cha kidijitali cha sasa, kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wanaotaka huduma bora, za uhakika na zinazotolewa kwa gharama nafuu.
Maeda ameeleza kuwa kifurushi hicho kimoja kinamuwezesha mteja kupata huduma ya intaneti ya kasi, simu ya mezani kupitia miundombinu ya faiba, pamoja na huduma ya simu ya mkononi yenye GB na dakika za kutosha kutumika popote pale mteja alipo.
Amesema huduma hiyo ni suluhisho kamili kwa familia, ofisi na biashara, kwa kuwa inarahisisha maisha, inapunguza gharama na inatoa thamani kubwa zaidi kwa wateja.
Aidha, amebainisha kuwa TTCL inalenga kuhakikisha kila nyumba, kila ofisi na kila mfanyabiashara nchini anakuwa sehemu ya mageuzi ya kidijitali, sambamba na kuunga mkono ajenda ya serikali ya kukuza uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya TEHAMA.



