
NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
KATIKA kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, viongozi wa dini kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga wameazimia mambo saba muhimu, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, kutumia busara na kuzingatia haki katika kipindi hiki nyeti kwa Taifa.

Viongozi hao walikutana kwenye Kongamano la Amani lililofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) – Uhuru Hosteli, Moshi huku Washiriki walikuwa ni maaskofu, masheikh,Mapadri,Wachungaji pamoja na viongozi wa kamati za dini za vijana na wanawake.

Maazimio
Akisoma maazimio ya kongamano hilo, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kilimanjaro, Alhaj Awadh Lema, amesema wamekubaliana kuhamasisha wapiga kura kuhakiki taarifa zao na kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Azimio jingine ni kuendelea na makongamano ya amani kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha wameazimia kuwa ,Vyombo vya Dola kutumia hekima na busara katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa siku ya uchaguzi.

Pia wameazimia kuwa,Viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha waumini kuhusu haki na wajibu wao katika kulinda amani.
Vilevile wameazimia kuepuka uchochezi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Mbali ya hayo , wamependekeza ushiriki mpana wa viongozi wa dini katika vyombo vya maamuzi na utungaji wa sheria.
Sambamba na hayo yote pia wamekubaliana kuhimiza kila mwananchi kutambua kuwa kulinda amani ni wajibu wake, hata anapodai haki.
Kauli za Viongozi wa Dini
Sheikh Shaban Mlewa, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, amesitiza kuwa amani ni tunu adimu ambayo ikipotea ni vigumu kuirudisha, akitoa mfano wa nchi zilizojikuta kwenye machafuko baada ya uchaguzi.
“Ni muhimu Watanzania kuwa wazalendo, kupendana, kusameheana na kuwa waadilifu ili kuendeleza utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Sheikh Shaban Juma, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, alieleza kuwa hakuna haki bila amani, akisisitiza kuwa msingi wa amani ni kumtambua Mungu, kutambua thamani ya nafsi yako na kulinda haki za wengine.
Wakili Mchungaji Daniel Swai, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini, alihimiza kila Mtanzania kutimiza haki yake ya kupiga kura na kulinda haki hiyo kwa njia ya amani.
“Ni kosa kubwa kuhamasisha watu kutotimiza wajibu wao wa kikatiba. Haki na amani ni mambo yanayokwenda pamoja,” alieleza.
Padri Deogratius Matiika, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Moshi, alisema haki ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesisitiza heshima kati ya wananchi na viongozi, na kukemea tabia ya kutoa matusi kwa viongozi kupitia mitandao ya kijamii.
Naye Padri Francis Mahimbo, kutoka Kanisa la Anglikana – Dayosisi ya Tanga, alihimiza kujengwa kwa jamii yenye kuvumiliana, akisema:
“Msingi wa amani ni haki. Taifa lisilolinda haki za watu wake haliwezi kuwa na utulivu wa kweli.”
Wito kwa Watanzania
Katika kongamano hilo, viongozi wa kamati za dini za wanawake na vijana walitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki uchaguzi kwa utulivu, kujiepusha na vurugu na kuwakataa wale wanaochochea uvunjifu wa sheria.

