NA MWANDISHI WETU, IRINGA
JUKWAA la Elimu ya Fedha, Huduma Jumuishi za Kibenki, Utunzaji wa Manzigira na Nishati Safi ya Kupikia linalosimamiwa na Benki ya NMB, limeendelea kupasua anga kuwaendea wananchi wa vijiji zaidi ya 2,000 visivyofikiwa na huduma hizo nchini, ambako wikiendi iliyopita ilikuwa zamu ya Wilaya za Iringa na Same.

Wilayani Iringa, jukwaa hilo maarufu kama ‘NMB Kijiji Day’ limeunguruma kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Itunundu iliyopo Pawaga, huku wilayani Same likifanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Ndungu, ambako Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Mamndolwa Gembe, alikuwa mgeni rasmi.

Katika NMB Kijiji Day Ndungu, Katibu Tawala Gembe ambaye alikuwa akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, aliishukuru NMB kwa kupeleka programu hiyo chanya kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wake, aliowataka kuchangamkia fursa za Elimu ya Fedha waliyopewa.
Mbele ya Meneja wa NMB Tawi la Same, Saad Maswila, Gembe aliwasisitiza wananchi na washiriki wa semina iliyoendeshwa kupitia programu hiyo kujipanga kwa mabadiliko, huku akiiomba NMB kuendelea kusambaza Elimu ya Fedha vijijini, sambamba na kubuni bidhaa rafiki zinazoendana na makundi yote ya kijamii.

Kutoka Itunundu, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Happiness Pimma, ambaye pia ni Meneja wa NMB Tawi la Mkwawa mjini Iringa, aliwahakikishia wananchi wa Tarafa ya Pawaga kuwa, benki yake ni mshirika sahihi wa ndoto zao za kukua kiuchumi.
Pima aliwataka wananchi hao kuitumia benki yake katika kuharakisha hatua za kimaendeleo na kwamba ujio wa NMB Kijiji Day katika tarafa yao ni jaribio la taassisi yake katika kuona namna sahihi ya kubuni na kufikisha kwa wakazi hao bidhaa rafiki zitakazochagiza maendeleo, ikiwemo ufunguzi wa tawi.

“Ujio wa Kijiji Day hapa ni katika kuiishi kaulimbiu yetu ya; Karibu Yako, tuko hapa kuwapa Elimu ya Fedha na Huduma Jumuishi za Kibenki, ukiondoa mbio za taratibu na michezo mbalimbali, lakini tumewaletea darasa linaloenda kuwaongezea uelewa wa masuala ya fedha.
“Semina hii itawafungulia fursa pana juu ya huduma za mikopo, bima mbalimbali zikiwemo za afya, majanga ikiuwemo moto, kama mlivyoona kwenye vyombo vya habari hivi karibuni tukiwapa fidia wafanyabiashara wa waliounguliwa bidhaa zao katika Soko la Mashine Tatu, ambao walikata bima na NMB,” alisema.
Akifunga Semina ya NMB Kijiji Day, iliyoendeshwa na Meneja Mauzo wa NMB Makao Makuu, Casto Mamboleo, aliyewapitisha washiriki katika mada mbalimbali ikiwemo Umuhimu wa Kuzingatia Bajeti, Matumizi, Akiba na Uwekezaji, Pimma aliwataka washiriki kuwa mabalozi wa benki yake kwa jamii inayowazunguka.
Naye Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza (SSP) Jawadu Abdallah, ambaye pia ni Mkuu wa Gereza la Pawaga, aliipongeza NMB kwa namna inavyojitoa katika kutanua ufahamu wa masuala ya fedha na bima, na kwamba anaamini ujio wa Kijiji Day Pawaga, utachochea maarifa ya kukua kiuchumi kwa wananchi.
Awali, Ofisa Tarafa wa Pawaga, Emmanuel Ngabuji, alisema NMB Kijiji Day ni tukio linaloenda kuacha alama kubwa mioyoni mwa wakazi wa tarafa yake na kwamba anaamini litakuwa jukwaa lenye manufaa makubwa kiuchumi na kiafya sio tu kwa wananchi wa Itunundu, bali tarafa nzima ya Pawaga.
NMB Kijiji Day Pawaga ilianza kwa mbio za taratibu ‘jogging,’ kisha michezo mbalimbali kuchukua nafasi ikiwemo Kuvuta Kamba, Mbio za Magunia, Kufukuza Kuku na kumalizia na mpira wa miguu, ambako Itunundu FC waliwachapa Mbuyuni FC ya Mbuyuni kwa bao 1-0 katika fainali.

