NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM

JUMLA ya wafanyabiashara 28 ambao pia ni wateja wa Benki ya NMB wanatarajiwa kusafirishwa kwenda nchini China kwa ajili ya mafunzo ya kibiashara, kutembelea masoko na kukutana na wenzao wa kimataifa ili kujenga mitandao ya biashara.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao iliyofanyika makao makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam,Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki hiyo, Filbert Mponzi, amesema safari hiyo ni sehemu ya jitihada za NMB kuwawezesha wateja wake kupitia mafunzo ya kimataifa.

Mponzi amesema safari hiyo ni ya tano kufanywa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake kutoka sekta mbalimbali ikiwemo biashara na kilimo, na mwaka huu idadi ya washiriki imeongezeka zaidi kuliko miaka iliyopita.
“Kati ya wafanyabiashara 28 wanaosafirishwa, 12 wanahusiana moja kwa moja na mnyororo wa thamani wa kilimo, huku wengine 16 wakitoka katika sekta nyingine,” amesema Mponzi.

Ameongeza kuwa safari hiyo itaanza Oktoba 15 na kumalizika Oktoba 24,2025, ambapo washiriki watapata nafasi ya kutumia SME Debit Card maalum zinazotolewa na NMB kwa kushirikiana na MasterCard.
“Kadi hizi zinawawezesha wateja kuingia kwenye maeneo maalum kama viwanja vya ndege, kuwa na bima ya kusafiri, pamoja na manufaa mengine. Bima hii inatoa kinga ya matibabu hadi dola 100,000 wakiwa nje ya nchi, fidia ya hadi dola 1,500 endapo mizigo itapotea, na dola 300 iwapo mizigo itachelewa kufika pia ikitokea safari imeahirishwa, mteja anaweza kupata fidia ya hadi dola 3,000,” amefafanua Mponzi.

Aidha, amesema wafanyabiashara hao watashiriki kwenye maonesho ya kibiashara nchini China, kutembelea wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, na kujifunza mbinu mpya za kukuza biashara zao.
“Mtapata nafasi ya kuangalia masoko mapya, kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa China ambao baadhi yao tayari wanafanya biashara nchini Tanzania hii itapanua zaidi mtandao wenu wa kibiashara,” ameongeza.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara waliowahi kunufaika na programu hiyo, Award Mpandila na Donald Philemon, wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kukuza ubunifu na biashara zao.
Mpandila ameema safari hiyo ilimpa ujuzi uliomsaidia kubuni betri aina ya Chui zinazotumika kwenye pikipiki na magari, huku Philemon akisema amefanikiwa kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa maji ya kunywa.
Miongoni mwa wafanyabiashara wanaotarajiwa kusafiri mwaka huu, Delphina Shime, ambaye ni mstaafu anayejishughulisha na kilimo, amesema anatarajia kutumia safari hiyo kujifunza zaidi kuhusu mbinu za kilimo cha kisasa na kutafuta fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara.
“Ni fursa kubwa sana kwangu. Naishukuru Benki ya NMB kwa kutuamini na kutuwezesha kupata ujuzi huu muhimu utakaotusaidia kuboresha biashara zetu,” amesema Shime.

