NA MWANDISHI WETU, MKURANGA,PWANI
PROGRAMU Endelevu ya usambazaji wa Elimu ya Fedha, Huduma Jumuishi za Kibenki, Utunzaji Mazingira na Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi vijijini ‘NMB Kijiji Day,’ imeendelea wikiendi iliyopita katika Kata ya Kimanzichana, wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
NMB Kijiji Day inayoendeshwa na Benki ya NMB na mshirika wake wa kimkakati, Kampuni ya Taifa Gas, inalenga kufikisha Elimu ya Fedha, Huduma Jumuishi za Kibenki kwa wananchi wa vijiji zaidi ya 2,000 visivyofikiwa na Huduma za Benki, ikijumuisha upandaji miti na bonanza la michezo mbalimbali.
Akizungumza na washiriki wa Semina ya programu hiyo, Meneja wa Kanda, Mauzo ya Vikundi na Huduma za Kibenki Vijijini wa NMB Makao Makuu, Dismas Prosper, alivitaka Vikundi vya Kijamii, wananchi na wajasiriamali, wakiwemo mama lishe na bodaboda, kuchangamkia fursa za Akaunti ya Vikundi.
Prosper aliwataka washiriki hao kuvirasmisha vikundi vyao kwa kufungua NMB Kikundi Akaunti, ili kunufaika na huduma za Bima, Mikopo na Huduma Jumuishi za Kifedha Kidigitali na kuharakisha maendeleo yao na ukuaji kiuchumi.
“NMB Kikundi Akaunti inajumuisha huduma chanya mbalimbali zinazoweza kuharakisha ukuaji kiuchumi wa vikundi na mwanachama wake, muhimu kwenu ni kuhakikisha mnakopa kwa mnakopa kwa malengo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya vikundi na wanachama mmoja mmoja.
“Akaunti hiyo ndio suluhisho la utunzaji fedha za vikundi, inayomwezesha kila mwanachama kujua namna ya kunufaika na pesa zake na kumsaidia mwanachama mmoja mmoja na vikundi kwa ujumla kufikia malengo na mipango katika matumizi ya pesa zenu.
Alibainisha ya kwamba, faida za NMB Kikundi Akaunti ni pamoja na usalama wa pesa za vikundi, ufunguzi na uwekaji akiba rahisi kidigitali, kupata taarifa sahihi na za wazi za kifedha kwa kila mwanachama na kusisitiza kuwa.
Akaongeza ya kwamba, licha ya akaunti za kikundi, wanachama wa Vikundi vya Kijamii wanapaswa kujifungulia akaunti binafsi ili kunufaika na huduma mbalimbali, ikiwemo Mshiko Fasta, mkopo usio na masharti, dhamana wala ujazaji fomu unaoweza kumpatia mteja wao hadi Sh. Mil. 1
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Idara ya Muzo wa Kampuni ya Taifa Gas, Henry Muya akizungumza na washiriki hao, alisema kampuni yake imejipanga vya kutosha kuhakikisha Elimu ya Utunzaji wa Mazingira na Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia inawafikia wananchi wote mijini na vijijini.
Muya alisema wananchi, hususan waishio vijijini wanapaswa kuamka na kutambua kuwa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia sio tu kwa wakazi wa mijini, bali kwa kila mtu, ili kuhakikisha wanaepuka madhara yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa ambayo huzalisha uharibifu wa mazingira.
Akizungumzia mafunzo na elimu ya fedha waliyopewa katika semina hiyo, Abdallah Omar, alikiri kuvutiwa na NMB Kikundi Akaunti na hata Bima za Vikundi, huku akiishukuru NMB na kuitaka kuongeza kasi katika kuvifikia vikundi vya kijamii vya watu walioko vijijini.
“Huku tuliko ndiko viliko vikundi vingi vya kijamii, tayari sisi ni wanufaika kwa sababu kupitia semina hii tumeweza kutambua namna sahihi ya kutunza pesa zetu kisasa, manufaa tunayoweza kupata kwa kurasmisha vikundi vyetu, lakini zaidi ni ile bima ya vikundi inayoweza kutoa mkono wa pole mtu anapofiwa,” alisema.
Naye Mariam Suleiman, aliyejitambulisha kama mwanachama wa Kikundi cha Wanawake na Maendeleo Kimanzichana, alisema amevutiwa na elimu juu ya huduma za Bima ya Afya ya Vikundi waliyopewa katika semina hiyo, hasa ukizingatia changamoto kubwa kwa wakazi wa vijijini ni uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Kupitia semina hiyo, mada mbalimbali za Sekta ya Fedha, ikiwemo mikopo nafuu na Bima zilitolewa kwa washiriki na Meneja Mauzo – Benki Vijijini wa NMB Makao Makuu, Robert Mtimba, ambaye pia aliwataka washiriki hao kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuharakisha ukuaji wao kiuchumi.