NA FLORAH AMON,PWANI

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema kuwa utekelezaji wa mafunzo ya Amali kwa shule za Sekondari umekuwa na mwitikio chanya kwa wanafunzi katika kujipatia ujuzi na maarifa na kuwaongezea fursa za ajira mara baada ya kuhitimu.

Akizungumza alipotembelea shule za amali mkoani Pwani na jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTVET, Bernadetta Ndunguru, amesema kuwa NACTVET imeendelea kutekeleza jukumu la kusimamia ubora wa mafunzo katika shule hizo kwa lengo la kuzalisha wahitimu wenye ujuzi stahiki.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa ya Dk.Samia Suluhu Hassan, imewekeza kikamilifu katika mafunzo ya Amali na matunda yake yameanza kuonekana kupitia kazi mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi wanaonufaika na mafunzo hayo katika shule mbalimbali nchini.

“Dhamira ya Serikali ya kuanzisha Mkondo wa Amali katika shule za Sekondari ni kuwandaa vijana kuwa na ujuzi katika fani mbalimbal,utakaowajengea msingi wa kujipatia ajira mara baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari ,” amesema
Kwa upande wake, Meneja wa NACTVET Kanda ya Mashariki, Dk.Hirst Ndisa, amesema kuwa NACTVET inaendelea kushirikiana kwa karibu na shule hizo ili kuimarisha ubora na ufanisi wa utoaji mafunzo.
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam, Hussein Njau, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha utoaji wa mafunzo ya amali ambayo yamekuwa chachu kwa wanafunzi kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

Mwanafunzi wa fani ya Ufundi Umeme katika shule ya Sekondari Baobab, Careen Jonathan, amesema kuwa kupitia mafunzo ya amali anaamini kuwa atakuwa na uwezo wa kufanya kazi mbalimbali za kitaalamu katika fani hiyo mara baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne.
Ameongeza kuwa kadri wanavyoendelea na mafunzo hayo, wanazidi kupata umahiri na ujuzi katika fani zao, jambo linalowasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii na hivyo kujipatia fursa za ajira.

