NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kuwa jumla ya vituo vya kupigia kura 99,911 vitatumika katika zoezi la kupiga kura wakati wa uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Agosti 1,2025 na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Ramadhani Kailima wakati wa mkutano wa kitaifa wa INEC na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kailima amesema Kati ya vituo hivyo, vituo 97,349 vipo Tanzania Bara na vituo 2,562 vipo Tanzania Zanzibar na kwamba vituo hivyo no ongezeko la vituo 18,344 kutoka vituo 81,567 vilivyotumika wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Aidha amesema kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na 4 ya mwaka 2024, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar huwa inafunga daftari la wapiga kura siku saba baada ya uteuzi wa Wagombea wa uchaguzi.
Hivyo amesema kwa kuwa uchakataji wa wapiga kura bado unaendelea kufanywa za ZEC, iwapo takwimu zitabadilika wadau wote watajulishwa.
Aidha amesema kwa mujibu wa kifungu cha sheria tajwa idadi ya vituo 1,766 vilivyopo sasa kwa mujibu wa daftari la wapiga kura la ZEC, ni sehemu ya vituo vitakavyotumiwa na INEC kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na wabunge kutoka Zanzibar.
“Katika vituo hivyo kuna vituo viwili vya Magereza kwa Tanzania Bara na kimoja cha Chuo cha Mafunzo kwa Tanzania Zanzibar ambavyo havikuandikisha wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari,” amesema Kailima
Kuhusu Majimbo, Kailima amesema INEC imekamilisha zoezi la ugawaji wa majimbo ya uchaguzi ambapo majimbo mapya nane yameanzishwa na M,ajimbo 12 yamebadilishwa majina kwa Tanzania bara.
“Hivyo idadi ya majimbo kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni 272 ambapo kwa Tanzania bara yapo majimbo 222 na Tanzania Zanzibar yapo majimbo 50,” amesema Kailima
Amesema jumla ya kata 3,960 zitatumika kwenye uchaguzi wa adiwani kwa mwaka 2025 na kwamba hiyo ni ongezeko la kata nne ikilinganishwa na kata 3,956 zilizokuwa wakati wa uchaguzi mwaka 2020.