NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MJUMBE wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Peter Shimo smeitaja Mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea hasa kipindi hiki tunapoelekea msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2025/2026, ili kuongeza uzalishaji kwa wakulima.
Aidha, ameitaka Mamlaka kuongeza juhudi za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuimarisha uzalishaji wa mbolea nchini na kuhakikisha upatikanaji wake kwa wakati.
Sambamba na hayo Dk.Shimo ameonesha kuridhishwa na namna Mamlaka hiyo inavyotoa elimu kwa umma kuhusu mnyororo wa thamani wa mbolea kupitia Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Haya yamejiri wakati Dk.Shimo alipofanya ziara katika mabanda ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Agrami Afrika na kujionea shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo katika kuendeleza kilimo nchini.
Akiwa katika banda la TFRA Dk. Shimo amepongeza ubunifu na ushirikiano mzuri kati ya TFRA na taasisi mbalimbali chini ya Wizara ya Kilimo katika kuwawezesha wakulima kuongeza tija kupitia huduma za ugani na upatikanaji wa mbolea kwa wakati.
Kadhalika,Dk.Shimo alisisitiza suala la kukuza na kuendeleza ushirikiano na mahusiano mazuri baina ya taasisi za kilimo ili kumsaidia mkulima kuzalisha kwa tija na hivyo kuongeza kipato chake na taifa kwa ujumla.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana katika kusambaza elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kanuni bora za kilimo kwa wakulima wetu,” amesema Dk. Shimo.
Wakati huo huo Meneja wa Uhusiano, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TFRA,. Matilda Kasanga, amesema wananchi wengi wamejitokeza kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa Mamlaka tangu kuanza kwa maonesho hayo.
“Wakulima kutoka ndani na nje ya nchi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya mbolea na wanajiandikisha kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku ili kunufaika na huduma zitakazotolewa na serikali kupitia mfumo huo,” ameeleza Kasanga.