NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametaja maeneo mbalimbali ambayo Tanzania imekubaliana kushirikiana na Serikali ya Msumbiji ikiwemo ya kuanzisha vituo vya pamoja kwenye mipaka ya nchi hizo mbili, uboreshaji wa miundombinu ya barabara mipakani, biashara, uwekezaji pamoja na uanzishaji wa Tume ya pamoja ya kiuchumi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2025, Rais Samia amesema amekubaliana na Rais mwenzake wa Msumbiji, Daniel Chapo kuanzisha vituo hivyo vya pamoja kwenye mipaka ya nchi hizo ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Msumbiji.
Amesema kuanzishwa kwa vituo hivyo kutarahisisha ufanyaji biashara kwa watu wa Msumbiji na Tanzania na kuongeza kuwa wamekubaliana pia kuanzisha Tume ya pamoja ya kiuchumi ambayo itakuwa na kazi ya kufuatilia masuala mbalimbali ya kiuchumi yaliyokubaliwa na kuhakikisha inayasukuma kwa haraka ili kufikia malengo.
Rais Samia amesema kwa wamekubaliana pia kuendeleza miundombinu na ujenzi wa barabara za mipakani baina ya nchi hizo mbili ili kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
“Kwenye mzungumzo yetu tumekubaliana licha ya ujirani na uhusiano wetu mzuri katika kihistoria lakini ushirikiano wetu wa kiuchumi bado haujaenda sambamba na ushirikiano wetu wa kisiasa na kidiplomasia, katika eneo la biashara na uwekezaji tumekubaliana kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kati yetu ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali, wafanyakazi wadogo na wa kati kufanya kazi kwa urahisi,” amesema Rais Samia.
Amesema Tanzania na Msumbiji pia zimekubaliana kushirikiana katika kufanya tafiti za gesi kwa pamoja na kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali za bahari ikiwa ni pamoja na utalii, uvuvi na malighafi zingine za bahari.
“Pamoja na mambo mengine tumekubaliana kunazisha tume ya pamoja ya kiuchumi ambayo itakuwa na jukumu ya kufuatilia kwa karibu zaidi yale tuliokubaliana kushirikiana ili kukuza uchumi wetu kwa haraka haraka,” amesema Rais Samia na kuongeza
“Kwa upande wa miundombinu na usafirishaji, tumezungumzia umuhimu wa kuendeleza ujenzi wa barabara zetu zilizopo mipakani zinazounganisha nchi zetu mbili na kufanya mapitio ya mikataba wa mashirikiano wa usafri wa anga, kuimarisha usafiri wa bahari kupitia ziwa Nyasa na Mto Ruvuma,” amesema Rais Samia
Kuhusu kilimo, Rais Samia amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha tafiti za kilimo hasa zao la korosho kutokana nchi zote mbili kuwa na rasilimali zinazofanana.
Aidha amesema mbali na hayo nchi zote mbili zinaeneo kubwa la bahari ya hindi na fursa za utajiri unaotokana na uchumi wa buluu zikiwemo uvuvi, utalii, madini na usafirishaji hivyo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali za baharini kubadilishana uzoefu na kufanya kazi kwa ukaribu kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu, utalii na usafirishaji.
“Ndio maana kesho Rais Chapo atatembelea Mamlaka ya Usimamizi na Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na soko la samaki pale Malindi kule Zanzibar ili kujionea jitihada zinazofanyika katika eneo hilo,” amesema Rais Samia
Kwa upande wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo amesema mambo muhimu waliyokubaliana na mwenzake wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kuimarisha usafiri wa anga kwa mashirika ya ndege ya Msumbiji na Tanzania ili kutoa huduma kwenye miji mikubwa ya mataifa hayo.
Rais Chapo amesema wamezungumza kuhusu uwepo wa safari za ndege za kutoka Msumbiji hadi katika miji ya Tanzania na vile vile usafiri wa ndege kwenda katika miji ya Maputo na Pemba nchini Msumbiji.
“Mbali na usafiri wa anga, Tanzania na Msumbiji pia tumekubaliana kushirikiana katika eneo jipya la Uchumi wa Buluu,Msumbiji inafurahi kuona inaingia makubaliano na Tanzania ya kushirikiana katika eneo la madini na nishati ambapo nchi yangu ina utajiri mkubwa wa madini kwa sasa,” amesema
Kuhusu ushirikiano na Tanzania, Rais Chapo amesema wameamua kuwa na mikutano na viongozi wa mikoa ya mipakani ili kuleta ushirikiano na kukuza amani baina ya mikoa ya maeneo ya mipakani.
Rais huyo wa Msumbiji amesema ziara yake nchini Tanzania ni kuja kuona maeneo waliyokulia na kupambania Uhuru, kwani chama tawala cha Msumbiji, FRELIMO hakiwezi kusahau namna Tanzania ilivyoshiriki kuwaletea Uhuru.