NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
ASASI za Kiraia (AZAKi) zimewasilisha maoni ya ziada ya kuhakiki rasimu ya Dira Ya Taifa ya Maendeleo 2050 chini ya uratibu wa Foundation for Civil Society (FCS) kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira hiyo.
Akizugumza katika mkutano wa AZAKi leo Januari 10, 2025 jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge, ameipongeza Kamati hiyo kwa ushirikiano wao na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wameshiriki kikamilifu tangu kuanza kwa mchakato mzima mwaka jana, ambapo AZAKI zilitoa mapendekezo ya matarajio yao katika dira hiyo.
Ameongeza kuwa, Mchakato wa kupata Dira ya Taifa ya Maendeleo ni muhimu ambayo ni mwongozo wa nchi kufikia maono yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwa miaka 25 ijayo ikiwa ni sehemu muhimu katika kupanga maeneo ya utekelezaji.
“AZAKI ni wadau muhimu katika kuchagiza maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini. Tumekuwa tukishiriki kikamilifu katika uboreshaji na utekelezaji wa Sera, Sheria na Mifumo ya kiutawala, pia tumekuwa mstari wa mbele kuwezesha wananchi kutoa mawazo na maoni yao.”amesema Rutenge.
Kaimu Mwenyekiti Kikosi Kazi cha AZAKI Lucas Kifyasi amesema maoni ya rasimu hiyo yamepatikana kutoka vyanzo mbalimbali kwa njia ya dodoso la mtandaoni (digital survey tool)
Ameeleza kuwa, mapendekezo yaliyomo katika rasmu hiyo ni pamoja na huduma za uhakika za uzazi, kutokomeza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, Bima nafuu ya afya kwa wote, hifadhi ya jamii jumuishi na uboreshaji wa sekta ya elimu.
Aidha, Kifyasi amesema eneo la kutazamwa zaidi ni usalama wa chakula kwa Taifa, uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha kwa makundi yote vijijini na mijini angalau kati ya dola za Marekani elfu nane hadi 12,000. Pia amesisitiza umuhimu wa kulinda maadili na utamaduni,
kutatua changamoto za maendeleo ya sekta ya Michezo, Sanaa ya Ubunifu pamoja na Haki Miliki ili kulinda ubunifu kwa manufaa ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Stanslaus Nyongo, amepongeza juhudi za AZAKi katika kufanikisha kikamili maboresho ya Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kusema kuwa Serikali ipo tayari kuyafanyia kazi ili kupata Dira kamili itakayokidhi maeneo yote kwa mustakabali wa maendeleo endelevu ya nchi na watu wake kwa ujumla kulingana na mabadiliko ya zama za sayansi na teknilojia.
Dira hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo teknolojia inakua kwa kasi sana na elimu ndiyo nyenzo muhimu ya uzalishaji wataalamu wa teknolojia kwa tija.