NA DANSON KAIJAGE,BAHI
UONGOZI wa wavuvi wa Samaki katika Mwalo wa Chali Isanga katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma,wamesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea machafuko katika Mwalo huo kutokana na wavuvi haramu kutoka Wilaya ya jirani ya Manyoni kuingia eneo hilo kuvua samaki kwa kutumia nyavu aina ya kokolo inayosababisha kuvua samaki wachanga pamoja na kuharibu nyavu za wavuvi wa Mwalo husika huku viongozi wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Chali wakiwa hawatoi ushirikiano.
Kutokana na kuhofia kutokea machafuko katika Mwalo huo Uongozi wa wavuvi umeiomba Serikali ya wilaya hiyo kuingilia kati mgogoro unaoendelea kati ya Wavuvi wa Mwalo huo na wale wanaotoka katika wilaya ya jirani ya Manyoni ambao wanaingia na kusababisha uharibifu wa nyavu zao na kuvua samaki wasiostahili yaani uvuvi haramu.
Malalamiko hayo yametolewa na Mwenyekiti wa wavuvi wa Mwalo huo Augustine Mtunya,Katibu wa Wavuvi wa Mwalo huo Daudi Kimwaga na mmoja wa wavuvi Heroati Dominick walipokuwa wakizungumza na wavuvi wenzao pamoja na Vyombo vya Habari.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kutokana na wavuvi kutoka wilaya ya jirani kuingia katika eneo lao la uvuvi na kuanza kuvua huku wakiharibu nyavu zao kunaweza kusababisha machafuko yanayoweza kuhataraisha usalama wa wavuvi katika eneo hilo.
“Kumekuwepo na mwingiliano wa wavuvi kutoka Wilaya ya Manyoni kuvua katika maeneo ya mwalo wetu wa hapa Chali Isanga mbaya zaidi wao wanavua kwa kutumia mitumbwi inayotumia mashine na sisi tunatumia mitumbwi ya makasia.
“Sisi tunaoendeleza uvuvi katika eneo hili tunafuata utaratibu na tunatumia nyavu zinazokubarika ambazo zinazingatia uvuvi sahihi lakini,lakini kinachosikitisha na kukatisha tamaa ni pale wenzetu ambao wanatoka upande wa manyonyi na kuvua kwa makokolo.
“Kinachotuumiza zaidi ni pale ambapo wanakata nyavu zetu na tukiwaambia wanatufanyia vurugu wanatutukana na kutuona kama hatuna akili jambo ambalo linatufanya kufikiri kinyume na ustaarabu”ameeleza Mwenyekiti.
Kwa upande wake katibu wa mwalo wa Chali Isanga Wilayani Bahi ,Daudi Kimwaga amesema kuwa uongozi wa Wilaya ya Bahi wanatakiwa kuingilia kati huo ngogoro kwani unaweza kusababisha machafuko.
“Tumepeleka malalamiko kwa viongozi wa Halmashauri,Diwani wa Kata lakini Bado hakuna juhudi zozote za makusudi za kutatua tatizo hilo.
“Kwa sasa katika kata ya Chali Isanga uchumi umeshuka kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya wavuvi kuchaniwa nyavu zao na wavuvi haramu wanaotoka upande wa Wilaya Manyoni.
“Kwa upande wetu hatuwezi kufanya doria kwenye maji kutokana na kutumia mitumbwi ya mparazo kwani wenzetu wanatumia mitumbwi ya kutumia mashine,hivyo tunaomba serikali kuingilia kati vinginevyo kuna uwezekano wa kutokea uvunjifu wa amani na kupelekea uchumi wa kata na halmashauri husika kushuka”ameeleza Kimwaga.
Naye mmoja wa Wavuvi wa Mwalo huo Heriati Dominic amesema yeye ni mmoja wa wahanga wa kukatiwa mitego yake ndani ya maji na wavuvi haramu kutoka wilaya ya Manyoni.
“Kuna mitego yangu ya ndoano ambayo uitega katika naji lakini hawa wenzezetu wakipita na makokolo yao wanavuruga na kukata mitego yetu na wakati mwingine kukokola hata samaki ambao tayari tunakuwa tumewatega”ameeleza mvuvi huyo.
Kwa upande wake wake Ofisa uvuvi wa kata ya Chali isanga Wilaya ya Bahi Hemed Ibrahim, amethibitisha kuwepo kwa wavuvi kutoka Wilaya ya Manyoni ambao wanatumia makokolo na kuvua samaki ambao hawastahiri kuvuliwa.
Akizungumza wananchi pamoja na Waandishi wa Habari waliofika katika mwalo bubu ambao utumiwa na wavuvi hao haramu amesema kuwa nyavu ambazo zinatumiwa hazikubariki kwani zinasababisha kuvua watoto wa samaki na kuharibu mazalia ya samaki.
“Uvuvi unaotumiwa na wavuvi ambao wanasemekana kuwa wanatoka Wilaya ya jirani ya Manyoni unakiuka utaratibu na sheria ya uvuvi kwani wanahatarisha maisha ya samaki pamoja na mazalia yake.
“Sisi tupo kwa ajili ya kupambana na hatua hiyo lakini tunakabiliwa na changamoto ya vifaa vya kufanyia dolia wao hao waharibufu wanatumia mitumbwi ya mashine na sisi tunatumia mitumbwi ya kupalaza hivyo ni shida kukabiliana nao”ameeleza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chali Isanga ambaye naye anatuhumiwa kwa kuchochea mgogoro huo Pius Ndoje alipotafutwa hakuweza kutoa ushirikiano licha ya kuwapigia simu maafiasa uvuvi na kuwataka wavuvi haramu hao kuachiwa huku akihaidi kuwa atashughulikia suala hilo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Bahi Donald Mejitii alipoulizwa juu ya kuwepo kwa mgogoro huo ameema ni kweli anaujua na Halmashauri inafanya utaratibu wa kuweka Boti za Doria
“Mgogoro huo tunaujua lakini hupo chini ya uongozi wa Diwani wa kata husika hata vivyo tumefanya mazungumzo kati ya mwenyekiti wa halmashauri ya manyoni ili kuona ni jinsi gani ya kutatua mgogoro huo”ameeleza.