NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa ni muhimu kufanya usafi kwenye fukwe mbalimbali na kutunza rasilimali za bahari ili ziweze kutumika katika kuleta maendeleo kwa jamii na nchi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Koncept Group, Krantz Mwantepele wakati alipokuwa akifanya usafi na wadau wa mazingira katika ufukwe wa Kawe uliopo jijini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo inayojishughulisha na matangazo ya kidijitali, masoko na mahusiano ya umma nchini, imefanya usafi huo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni yao ya Okoa Bahari iliyoanzishwa zaidi ya miaka sita iliyopita kwa lengo la kuendeleza matumizi sahihi ya habari na kuangalia changamoto zinazoikumba.
Mwantepele amesema bahari ni chanzo muhimu cha uchumi kwa Tanzania na dunia kwa ujumla hivyo wadau hasa wa mazingira hawana budi kukitunza ili kiweze kutumika kuleta maendeleo katika jamii.
“Tunapata chakula kupitia samaki wa baharini, lakini mabadiliko ya hali ya tabia nchi yanachangia bahari kuharibika ili tuweza kukabiliana na jambo hilo inatupasa kuhakikisha tunatunza fukwe zetu na kuzilinda rasilimali za bahari ili zichochee ukuaji wa uchumi.
“Koncept kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mzingira tutaendelea kuhakikisha kampeni yetu ya okoa bahari inafanikiwa hasa katika kuhamasisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya bahari na kutengeneza mazingira ya bahari kuwa rafiki ili yaendelee kuchochea uchumi,” amesema
Aidha amesema kila mwisho wa mwezi watakuwa wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya fukwe na maziwa lengo ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uharibifu na matumizi mabaya ya bahari yanavyoleta athari kubwa katika maisha ya watu kiujumla.
“Tunataka kuhakikisha watu wanaotumia mazingira ya bahari wanakuwa mstari wa mbele kuyaboresha na kuzuia yasiharibiwe, tunaendelea kuandaa kampeni mbalimbali zinazohamasisha matumizi sahihi ya bahari,” amesema
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzimuni Kawe, Raiya Nassor amesema fukwe za Tanzania ndio utalii wake ni muhimu zikatunzwa kwa kufanyiwa usafi mara kwa mara.
“Fukwe ya hapa Kawe ndio utalii wetu maana wageni mbalimbali wanakuja hapa kununua samaki, kupunga upepo na wengine kuogelea, kwa kutambua umuhimu huo kila wiki tumekuwa tukifanya usafi ili kiuhakikisha inakuwa na mazingira mazuri ya kuvutia,” amesema Nassor


