NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
ZAIDI ya Wadau 1500 kutoka Mataifa mbalimbali duniani wanatarajia kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa lengo la kubadilishana mawazo na kujadiliana namna nzuri ya kuendeleza sekta hiyo hasa kwenye masuala ya teknolojia na uongezaji wa thamani.
Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21 Mwaka huu jijini Dar es Salaam ukiwa na kauli mbiu ya ‘Uongezaji thamani madini kwa lengo la kukuza na kuboresha maendeleo ya jamii kiuchumi’.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo katika kikao cha maandalizi kuelekea mkutano huo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Tanzania ipo tayari kwa ajili ya uongezaji thamani madini na kupitia mkutano huo wanawakaribisha wale wote ambao wapo tayari kushirikiana nao katika jambo hilo.
Amesema Wizara ya Madini kwa kutambua kwamba sekta ya madini ni muhimu hapa nchini imeandaa mkutano huo ambao utakusanya wataalamu, wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Aidha Mavunde amesema ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ni lazima kuongeza thamani madini yetu ili nchi iweze kunufaika na rasilimali hio ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia taifa la Tanzania.
“Tunafahamu kuwa ukiongeza thamani madini ndani ya nchi utaiongezea nchi mapato, utaongeza nafasi za ajira na mzunguko wa fedha unakuwa mkubwam hiyo ndio dhamira ya Rais Samia,” amesema na kuongeza
“Mwaka 2017 ilishuhudia mabadiliko ya sheria ambayo yaliweka takwa la lazima la uongezwaji thamani wa madini ndani ya nchi, mwaka huu kauli mbiu ya mkutano inajielekeza katika kuiambia dunia kwamba Tanzania ipo tayari kwa ajili ya uongezaji thamani madini na kuwakaribisha ambao wapo tayari kushirikiana nasi katika jambo hilo,” amesema
Amesisitiza kuwa sekta ya madini imeendelea kukua mwaka hadi mwaka huku mchango wake katika pato la Taifa kwa mwaka 2021/2022 ukiwa asilimia 6.7 na mwaka 2024 ni asilimia 9.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Benjamin Mchwampaka amesema baadhi ya nchi ambazo zinahusika na uchimbaji wa madini zinatarajiwa kushiriki katika mkutano huo ni Austalia, Canada, Afrika Kusini, Marekani, Ghana pamoja na Urusi.
“Lengo letu katika mkutano huu ni kuhamasisha uongezwaji wa thamani wa madini nchini, pamoja na kuhamasisha sheria, kanuni na sera zinazotungwa zinaweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji katika sekta ya madini,” amesema
Mchwampaka amesisitiza kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utatoa fursa kwa Tanzania kunadi utajiri wake wa madini ambao umebarikiwa na Mungu.