NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA a Bima la Taifa ( NIC INSURANCE) kupitia Bima yake ya Maisha limekuja na huduma ya mkopo midogo midogo na ya muda mfupi iitwayo Nisogeze
Sababu za kuanzishwa kwa huduma hiyo ambayo ni ushirikiano wa NIC Insurance na Benki ya Taifa ya Biashara (TCB) ni kutatua changamoto za muda mfupi za kifedha zinazowakabili wateja wa Bima za maisha.
Akizungunza na Demokrasia Digital Katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2024 jijini Dar es salaam,Ofisa Bima wa NIC Upendo Shengena amesema kigezo Kikuu cha kujiunga na Nisogeze ni kuwa na hati ya Bima ya Maisha kutoka NIC Insurance.
Shengena ameeleza kuwa wakati ambao mteja anaweza kuanza kunufaika na huduma ya Nisogeze ni kuchangia ada kuanzia mwezi mmoja .
Akielezea Bima za Maisha zinazotoa faida ya Mkopo wa Nisogeze Shengena amesema ni Bima ya malengo ya miaka 20,Bima ya maisha iliyoboreshwa ya miaka 10 au 11,Bima ya Matumaini(Flex) ya miaka 9 ,Bima ya Majaliwa ya miaka mitano na Bima ya maisha ya elimu ya miaka mitano na kuendelea.
Pia Shengena amesema kuwa ili kupata huduma hiyo mteja anapaswa kujaza fomu ya kuomba kujiunga inayopatikana kwenye Ofisi za NIC ,kwenye tovuti pamoja na Matawi yote ya Benki ya TCB.
“Mteja akitaks kuomba mkopo wa Nisogeze atafungua simu yake ya kiganjani na kubonyeza 150*44 kisha atafuata maelekezo ambapo kiwango cha mkopo kitategemea na kiasi cha akiba kilichopo kwenye Bima ya maisha ya mteja” amefafanua Ofisa huyo wa Bima
Katika hatua nyingine,amesema muda wa kurejesha mkopo wa Nisogeze ni matakwa ya mteja ingawa ni kuanzia saa 24 hadi miezi sita ambapo akimaliza kulipa mkopo wake anaweza kuomba mkopo mwingine lakini akishindwa kulipa hataweza kupata mkopo mwingine ila mkopo wake utakuja kulipwa mwisho wa mkataba kulingana na akiba aliyojiwekea kupitia Bima yake ya maisha.
“Iwapo mteja atafariki akiba yake ya Bima ya maisha haitaathirika kwa kuwa mkopo wake utafutwa na mafao ya Bima yatalipwa kwa mujibu wa utaratibu na sheria za mirathi.
” Na iwapo mteja atasitisha kuchangia Bima ya maisha hawezi kuendelea kupata mkopo wa Nisogeze kwa kuwa hatakuwa na akiba”amefafanua zaidi.
Akielezea tofauti ya Nisogeze na huduma zingine zilizopo sokoni,Shengena amesema Nisogeze inatoa jawabu la haraka kwa changamoto ya kifedha kwa wateja wa Bima za maisha kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu kwa kutumia simu ya mkononi sambamba kuwaondolea Wateja usumbufu wa gharama zitokanazo na mikopo.