NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kwa ukomo wa riba ya asilimia 6 katika robo ya tatu ya mwaka 2024 kati yake na Benki za biashara nchini.
Riba hiyo itatumika katika kipindi cha robo ya tatu kuanzia leo Julai 4,2024 hadi Septemba, mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Julai 4,2024 , Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dk. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, imeamua riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.
Amesema uamuzi huu umefikiwa katika kikao cha Kamati kilichofanyika Julai 3, 2024 na kwamba tathmini ya kamati kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba,utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia tano.
“Maamuzi ya kamati pia yanazingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia, ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.
“Aidha, Kamatii inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi, sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha, na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana na shughuli za utalii, pamoja na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula.” amesema
Dk.Kayandabila amesema, katika kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024.
Pia amesema mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sanjari na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na benki kuu katika nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba.
“Bei ya mafuta ghafi ilipungua, licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi Juni 2024. Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu, ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama uwekezaji mbadala katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani.” amefafanua
Amesema matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025, licha ya kuwepo kwa hatari ya kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara.
Kuhusu mwenendo wa Uchumi wa Tanzania, amesema kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza Uchumi.
Amesema hali hiyo ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, kufuatia hali nzuri ya hewa kwa ajili ya shughuli za kilimo, upatikanaji wa uhakika wa umeme, uboreshaji wa miundombinu (hususan reli, barabara, na bandari), pamoja na sera na programu za maboresho.
Hata hivyo amesema uchumi ulikua kwa asilimia 5.1 mwaka 2023, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka 2022 na kwamba ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, uchimbaji madini na mawe, ujenzi na shughuli za kifedha (hususan ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi).
“Aidha, shughuli za utalii, ambazo zinategemeana na sekta nyingine za uchumi zimeendelea kuchangia kuimarika kwa uchumi nchini. Kamati inakadiria ukuaji wa uchumi kuwa takriban asilimia 5 na 5.4, katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024, mtawalia,” amesema
Amesema mwenendo wa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara, ambapo ulikua kwa asilimia 7.4 mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2022.
“Mwenendo huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, huduma za chakula na uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi. Mwenendo huu wa ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na 2025,” amehutimisha