NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa mkopo wa Dola Bilioni 2.5 ambazo Tanzania imeupata kutoka Korea hauna masharti yeyote yale ya kuweka rehani rasilimali za Tanzania kama inavyosambazwa na mitandao ya kijamii.
Waziri Kitila amesema mkopo huo wala hauna masharti ya kutoa bahari na madini kwa Wakorea kama inavyosambazwa bali amesema ni mkopo ambao una faida kubwa kwa nchi.
Ameyasema hayo leo Juni 6, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara rasmi ya Kiserikali aliyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, jijini Seoul, Jamhuri ya Korea kuanzia Mei 31, 2024 hadi Juni 05, 2024.
Amesema mkopo huo walioupata si wa kwanza kupokea kutoka Korea na kusisitiza kuwa kukopa ni muhimu kwa sababu ni moja ya nyenzo za kujenga uchumi wa nchi, kujenga uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi wake muhimu tunakopa kupeleka wapi na kwa masharti gani.
“Huu siyo mkopo wa kwanza tunaupokea kutoka mataifa mbalimbali duniani, mmemsikia Waziri wa fedha akisema bungeni nchi yetu imeshakupa matrioni, na hakuna mkopo hata mmoja ambao tumewahi kupokea kwa maana ya kuweka rehani rasilimali yetu mojawapo hasa za asili, huu ni mkpo wa pili kupokea kutoka Korea tulikuwa tumekopa Bilioni 1.
“Sisi kama nchi tumeshajiwekea utaratibu kwenye sera zetu za kifedha namba moja ni kutumia kadiri iwezekanavyo mapato ya ndani na ndio maana tunapambana kuongeza uwezo wa ndani kwa maana ya mapato kupitia kodi ya watanzania, kipaumbele cha Tanzania kuchukua mikopo yenye masharti nafuu, na kwaajili ya kujenga uwezo wa nchi. Huu mkopo tutalipa kwa miaka 40 na riba yake ni asilimia 0.01 na utaanza kulipa baada ya miaka 25 tangu tulipopokea,” amesema
Aidha amesema wanazingatia sheria zote za nchi katika mikopo hiyo na kwamba fedha hizo zinakwenda katika maeneo ambayo yana tija na kuongeza kuwa watu wakiona Rais amesafiri kwenda nchi mbalimbali ni kwa faida ya watanzania na nchi kwa ujumla.