NA KASSIM NYAKI,DODOMA
BAADHI ya Wabunge wamepongeza juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini hasa kupitia filamu ya Tanzania the Royal Tour na amazing Tanzania iliyozinduliwa hivi karibuni nchini China.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Kagera Oliver Semuguruka amesema Juhudi za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta binafsi imechangia ongezeko la watalii wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 Mwaka 2023 na watalii wa ndani kuongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 mwaka 2023.
Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Kisangi amebainisha kuwa kupitia filamu ya Tanzania the Royal Tour idadi ya wageni wa nje wanaotembelea hifadhi zetu imekuwa kubwa na kutoa hamasa kwa watalii wa ndani kuendelea kuhamasishwa kutangaza vuvutio vya nchi yao na kuishauri Wizara na Taasisi zake kutengeneza filamu nyingi zaidi hasa ninazolenga kuhamasisha watalii wa ndani ili idadi iendelee kuongeza kama ilivyo watalii wa nje.
Katika kuboresha utoaji huduma bora kwa watalii wanaotembelea nchi yetu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida Martha Gwau ameishauri Serikali kuendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ukarimu na utoaji huduma bora kwa wahudumu wa hoteli, viwanja vya ndege, waongoza watalii, watumishi kwenye maoneo ya hifadhi kwa kuwa ndio wanaokutana kwa mara ya kwanza na wageni wanaotembelea nchi yetu.
“Tuendelee kuimarisha huduma ili wageni wanaokuja wawe na utamaduni wa kurudi mara ya mbili, baada ya Serikali kutangaza kwa juhudi kubwa utalii wetu wageni wanaokuja wanakutana na watoa huduma wa hoteli, madereva, waongoza watalii na wahudumu kwenye hifadhi zetu, lazima tusimamie mafunzo ya watumishi hawa ili wawahudumie wageni vizuri na kuwafanya warudi kila mara nchini kwetu” amefafanua Gwau.
Gwau ameishauri Wizara na wadau wa Sekta ya utalii kwa ujumla kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vya utalii sambamba na kuona uwezekano wa kuwa na afisa dawati/mwambata wa utalii katika balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali.
Kw upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu Tunza Mijika ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa bajeti yenye vipaumbele vya uhifadhi wa Wanyamapori, Mambo kale, misitu na nyuki pamoja na kutangaza vivutio vya utalii na kusisitiza kuwa jitihada za uhifadhi wa maeneo hayo ziendelee kushirikisha wananchi katika maeneo yao.