NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
BALOZI wa Ubelgiji nchini Tanzania Peter HuygheBaert ameonesha kuridhishwa na kazi inayofanywa na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA pamoja na Kituo cha Utafiti cha Mradi wa Apopo katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazozikumba nchi mbalimbali duniani ikiwemo kurudisha maeneo ya kuishi kwa usalama kupitia uteguzi wa mabomu.
Ameyasema hayo leo Mei 30, 2024 wakati akiwa kwenye ziara ya siku moja SUA kutembelea miradi yenye ufadhili wa taifa la Ubeligji ambapo amesema kupitia maelezo ambayo amepatiwa na wenyeji wake ameona tija ya miradi hiyo ambayo amekiri kuwa uwepo wake umekuwa katika manufaa kwa wananchi hasa mataifa yenye machafuko.
“Kile tulichokiona kinavutia sana kutokana na ushirikiano uliopo kwanza kabisa baina ya SUA na Chuo chetu cha Antwerp na baadaye kushirikiana katika Mradi wakuvutia sana wa kutumia Panya katika matumizi mbalimbali lengo likiwa kuifanya jamii kuwa salama”, amesema Balozi huyo.
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka SUA Prof. Abdul Katakweba akimuwakilisha Prof. Allen Malisa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Viumba Hai Waharibifu amesema APOPO inafanya kazi chini ya SUA lakini pia kuna ushirikiano baina ya SUA, APOPO pamoja na Chuo Kikuu cha Antwerp kilichopo nchini Ubelgiji.
Amesema APOPO ni Taasisi isiyo ya Kiserikali kutoka nchini Ubelgiji na huo ubalozi ndio unaofadhili sehemu kubwa katikika tafiti zinazofanyika na shirika hilo pamoja na SUA hivyo ujio wa balozi huyo ni kujiridhisha kwa kuangalia endapo misaada inayotolewa na nchi yao kama inafanya kazi vizuri na kitu kizuri ni kuwa kazi imeonekana.
“Ushirikiano wetu mkubwa kati ya APOPO na SUA ni ufanyaji wa Tafiti katika kusaidia binadamu wa ndani ya nchi na nje ya Tanzania ambapo tunatumia panya kunusa mabaomu lakini pia makoozi kwa ajili ya kubaini vimelea vya Kifua Kikuu na kwa upande wa Tanzania tafiti hiyo imekwenda vizuri sana ambapo tuna hospitali zaidi ya 58 ambazo panya hao wanaweza kutumia makoozi ili kuweza kubaini vimelea hivyo”, amesema Prof. Katakweba.
Katika Zira hiyo Balozi huyo ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Maabara ya kutambua vimelea vya Kifua Kikuu (Morogoro TB Detection), Shamba la Mfano la Mafunzo la Kilimo Msitu, Eneo la Mafunzo ya Panya wanaokabiliana na majanga ikiwemo kutegua mabomu na baadaYe kumalizia Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Chuo.