NA CATHREEN BUKUKU,MOROGORO
BALOZI wa Norway nchini Tanzania Tone Tinnes amefanya ziara katika Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine ( SUA)kilichopo mkoani hapa kukagua na kuangalia maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo wanayoifadhili.
Baadhi ya miradi hiyo ni uratibishwaji wa hewa ya Ukaa uzalishaji wa samaki aina ya Sato na Kambale na vyakula vyake,kilimo biashara cha kisasa cha pilipili hoho nyekundu na njano,nyanya na mazao mengine.
Miradi mingine ni mashamba ya malisho kwa ajili ya Ng’ombe wa maziwa ,Mbuzi wa maziwa na Kondoo.
Pia Balozi Tinnes kwenye ziara yake alitembelea baadhi ya Maabara zinazopatikana chuoni hapo na kuona vifaa kazi vinavyotumiwa na wanafunzi.
Akizungumza na Demokrasia Jumatano,Mkuu wa chuo cha Sokoine Profesa Raphael Chibunda alieleza kuhusu makubaliano walioweka kati ya SUA na Chuo cha Sayansi hai kilichopo Norway wakati Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipotembelea Norway Februari mwaka huu .
Prof Chibunda alieleza kuwa ndani ya makubaliano hayo moja wapo ni katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuwaandaa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,pili ni kuhusu kubadilishana uzoefu wa wataalamu kati ya vyuo hivyo viwili kama vile kubadilishana walimu,watafiti pamoja na wanafunzi ili kuwajengea uwezo zaidi.
Alibainisha kuwa Mradi huo wa hewa ya ukaa unahitaji takribani Dola za Kimarekani Milioni tano kwa kipindi cha miaka mitano ili kuutekeleza kwa ufasaha zaidi .
Kwa upande wake,Profesa Eliakiam Zahabu alisema,Pesa hizo zikipatikana zitawezesha pia wingi wa wanafunzi kujifunza zaidi kuhusu Hewa ya Ukaa au Kaboni kwakuwa mahitaji muhimu yatakuwa yamepatikana kuliko ilivyo sasa.
Katika hatua nyingine,Balozi Tinnes alipata wasaa wa kushukuru timu nzima ya ubalozi pamoja na chuo kwa maandalizi yaliyofanyika pamoja na kazi zinazoendelea kwenye miradi mbalimbali chuoni hapo na kuahidi ushirikiano huo kuendelea kufanywa na Ubalozi wa Norway na SUA.