- HILI linawasumbua, na hata kuwaumbua,
Watu wanawatambua, na wasiowatambua,
Nguo zao wawavua, bila wao kutambua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Wewe una kitumbua, mwenyewe wakichimbua,
Uongo wanaibua, wapate kukusumbua,
Maneno wanachukua, kuyasema yanakua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Watu wanakutambua, kwa uzuri wakujua,
Wao wanayaibua, hata wasiyoyajua,
Nguo zako wakuvua, wakubutua butua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Mengine wanayajua, hata wasiyoyajua,
Ya kwao wanayajua, na watu yawazuzua,
Wamekaa kutibua, na amani kuchukua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Mchumba memuibua, kwa mipango na hatua,
Hatua mnachukua, harusi ipate kua,
Watoka usikojua, mipango wanatibua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Mpenzi bila kujua, mapya yako anajua,
Bila ya kujisumbua, ukweli kuutambua,
Pete uchumba avua, sababu huwezi jua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Kwenye ndoa twawajua, wale wanajiinua,
Amani wakiijua, wawili mnaijua,
Wanakuja kubutua, mfike msikojua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Hata kazini hutua, hili lile kuchukua,
Lengo ni kuwatibua, kwa yale yanasumbua,
Uhasama unakua, bila wenyewe kujua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Mmbea nisokujua, Mungu yeye akujua,
Watu unawasumbua na maisha kutibua,
Unadhani wachanua, Mungu meshakugundua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani. - Ni muuaji tambua, pendo linalochanua,
Mtu ala kitumbua, kwa mchanga watibua,
Ujue umeshakua, Mungu atakuumbua,
Watu wambeawambea, ni hatari duniani.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602