- AONDOKA kaenda zake, zinabaki sifa zake,
Wanaume wanawake, wengi wanasema yake,
Hiyo ni alama yake, yabaki aenda zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Hiki umuhimu wake, acha niliseme peke,
Kwa Lowassa kazi yake, katika uhai wake,
Hili vema tutamke, kaacha alama yake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Shule za kata ni zake, wazo lake kazi yake,
Tufurahie tucheke, watoto waelimike,
Ni vema ifahamike, Lowassa kaenda zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Hali ilikuwa mbaya, Kikwete wakati wake,
Shule chache angaliya, watoto watawanyike,
Wawili hawakugwaya, sekondari wasimike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Uamuzi kila kata, iijenge shule yake,
Ni sekondari za kata, nchini tuzisimike,
Lowassa lipitapita, mtu asikengeuke,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Kwa sasa watoto wengi, hatutaki wachepuke,
Shule zimekuwa nyingi, lazima waelimike,
Tena na ajira nyingi, walimu waajirike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Sasa wahitimu wengi, kutokea shule zake,
Wapo waupiga mwingi, kiuchumi tuibuke,
Ni kwa ule umuhimu, zile jitihada zake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Mesoma shule ya kata, na Lowassa mkumbuke,
Jinsi alivyochakata, kwamba shule zijengeke,
Sasa ukipitapita, nyingi hata usitake,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Kitu akisimamia, ni lazima kifanyike,
Kama hujamjulia, utajua usitake,
Sasa ametangulia, mwache akapumzike,
Alifanya kazi yake,sisi twayala matunda. - Unazikwa mwili wake, na kuonekana kwake,
Walakini kazi zake, katika maisha yake,
Ni zetu siyo za kwake, zinabaki zitumike,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda. - Sasa yamekwisha yake, na ya kwetu tuyaweke,
Kesho tuje tutajike, majina tuyasimike,
Wajao wafaidike, nasi tukaongeleke,
Alifanya kazi yake, sisi twayala matunda.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602