- NATAFUTA marafiki, miongoni mwa wanangu,
Kwa mama hawabanduki, hata nikiwapa fungu,
Wanataka ipi kiki, ya kuwasogeza kwangu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Ada ninalipa mimi, kupitia kwa mwenzangu,
Na kitengo cha uchumi, hicho ni himaya yangu,
Iweje hawa wasomi, kwao niwe nyanya chungu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke - Tulipoenda likizo, mzigo likuwa kwangu,
Japo kulipia tozo, aliyefanya mwenzangu,
Na gharama zinginezo, bili yote juu yangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Wekundu wa Msimbazi, wengi wamejaa kwangu,
Japo mwenzangu mzazi, pia anayo mafungu,
Ila mengi matumizi, yako mabegani mwangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Simu zile za kisasa, kwa ajili ya wanangu,
Nilizinunua kosa, aliyewapa mwenzangu,
Mbona sasa wanitosa, na kunipiga majungu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Kuna wakati mwingine, wataka kampani yangu,
Nami kwa kazi zingine, ninamtuma mwenzangu,
Sasa ndio wanione, kama upepo kwa wingu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Niliagiza samaki, niitibu hamu yangu,
Nitafune na matoki, au chele la Usangu,
Na nyumbani sibanduki, nikisubiria changu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Samaki hawakuleta, hata wale wa mafungu,
Sebuleni wakapita, pasipo heshima yangu,
Hivi miye kwao Tata, au wa unga mzungu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Kuna siku nimepanga, tumtembelee Sangu,
Watoto wakaniunga, ikawa furaha yangu,
Mama yao akapinga, tutamaliza mafungu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Watoto wakageuka, safari kapigwa pingu
Ya mama yakayashika, wakayatosa ya kwangu,
Pamoja na kuumbuka, nilibaki na uchungu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Tena akafika ndugu, wa nyumbani kwa babangu,
Mke kamuona gugu, kamuwekea kiwingu,
Watoto zao vurugu, akalala kwa uvungu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Kesho yake aliaga, akiwa nje ya kwangu,
Ile simu alipiga, alisema kwa uchungu,
Na kwa kinagaubaga, kamwe hatakuja kwangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Watoto hawanitaki, wamuandama mwenzangu,
Ndugu zangu nao nduki, hawaji nyumbani kwangu,
Mbona mambo haya dhiki, kuzidi umri wangu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Kuwaonya nawaonya, kwani ni watoto wangu,
Mama yao kiwasonya, ndipo wanakuja kwangu,
Nikiwapa la kufanya, wadharau neno langu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Hivi niwafanye nini, wawe marafiki zangu,
Hebu nipeni maoni, mniondoe uchungu,
Hata lini hii soni, wakati nina wanangu?
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Natamani acha kazi, nikae nao wanangu,
Ndururu za matumizi, ndizo zanitia pingu,
Sipati usaidizi, kwake mzazi mwenzangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Kwenda kwa viti virefu, hiyo si tabia yangu,
Takaa muda mrefu, kuyapoteza mafungu,
Nilale kwenye sakafu, niugulie kivyangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Ni hekima toka zama, zile za wazee wangu,
Nafasi ya huyo mama, ni bora kuliko yangu,
Nabaki kushika tama, kama zee la kizungu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Watoto ona huruma, kwani nyie ni wanangu,
Pale ninapowatuma, sikiza sauti yangu,
Kama nyie mkigoma, tafupisha siku zangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Hata wewe mke wangu, nomba sinipe uchungu,
Kwa kuwateka wanangu, wasisikie ya kwangu,
Hebu umwogope Mungu, unanitia uchungu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Hii dunia ya leo, baba ninao uchungu,
Jinsi ninakosa cheo, kwa mke nao wanangu,
Nabaki kama pozeo, wakikula pesa zangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Mkituheshimu sote, mi na mzazi mwenzangu,
Mnazo baraka zote, pamoja na mali zangu,
Mtakuwa kwangu pete, kama ya huyu mwenzangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke. - Lakini na wewe baba, yasikupate ya kwangu,
Pamoja na kunikaba, pengine sababu yangu,
Nilitenga muda haba, kuwa na watoto wangu,
Jamani nishaurini, nisibakie mpweke.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB) lwagha@gmail.com