NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza Mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa yanayotarajiwa kufanyika wilayani Monduli mkoani Arusha Jumamosi Februari 17, 2024.
Awali Rais DkSamia alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia Februari 10, 2024.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumapilii, Februari 11, 2024 wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.
Amesema katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya Kitaifa na wanafamilia.
Amesema kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Amesema Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari Lowasa utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya Ibada Takatifu na kuagwa
Amesema Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Waziri Mkuu huyo mstaafu alifariki jana (Jumamosi, Februari 10, 2024) wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam na tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.