NA TIMOTHY ANDERSON
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na utekelezaji na usimamizi wa programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima nchini.
Programu hizo ni pamoja na Programu ya Elimu changamani baada ya Msingi (IPPE), Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya Mfumo rasmi (IPOSA), mradi wa kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari na programu ya Elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala (SEQUIP-AEP) pamoja na programu ya Elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala .
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo jijini Dar es Salaam tarehe 20 Januari, 2024, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mussa Ramadhani Sima amesema Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo baada ya kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kibajeti.
“Kamati imesikia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa miaka mitano katika eneo la elimu kwa njia mbadala pamoja na maeneo ya vipaumbele kwa miaka mitano ya baadae, ikiwemo kuhakikisha vijana wa kiume na kike ambao wamekatisha masomo kwa sababu mbalimbali wanarejea shule.’ amesisitiza Sima
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya maboresho ya sekta ya elimu kwa njia mbadala nchini na kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia ikiwemo miundombinu.
Aidha, Waziri Mkenda ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa kila kijana wa kike na wakiume ambae alikatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni.
Awali, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi ,ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za TEWW pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali kwa mustakabali wa maendeleo ya elimu kwa njia mbadala nchini.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo inaendelea na vikao vyake kawaida ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa kumi na nne wa Bunge utakaoanza siku ya Jumanne, Januari 30, 2024.