NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WATAALAMU wa Magonjwa ya Mfumo wa Mapafu na Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, leo Januari 22,2024 wamemtoa mama mwenye umri wa miaka 53, ganda la pipi kwenye pafu lake la kushoto kwa kutumia kifaa maalumu chenye kamera kilichopelekwa moja kwa moja hadi lilipo na kulinasa na kisha kulitoa.
Akizungumza baada ya kutoa ganda hilo, Daktari wa Magonjwa ya Mapafu na Mfumo wa Upumuaji, Dk. Hedwiga Swai amesema kuwa mgonjwa huyo alikuja akiwa na tatizo la mapafu yake kuharibika na kutoa usaha vilevile alikua anatoa makohozi yenya harufu kali.
“Mgonjwa huyo alikuja kwa lengo la kufanya vipimo vya kifua (Bronchoscopy) ila baada ya kuingiza kifaa chenye kamera kwenye mapafu tuliona kuna kitu ambacho sio cha kawaida katika pafu lake la kushoto na tulipoangalia vizuri tuligundua kuwa huo haukua uvimbe bali ni ganda la plastiki” amesema Dk. Swai.
Dk. Swai ameeleza kuwa mgonjwa huyo alikua anamng’unya pipi na ganda lake mwaka 2013 kwa bahati mbaya akameza na ganda lake na alipoenda hospitali hawakuona tatizo lolote na baada ya muda alianza kukohoa na kutoa usaha, ndipo alipoanza kutumia dawa za kutibu ugonjwa wa Kifua Kikuu bila mafanikio yeyote.
Dk. Swai ameitaka jamii kuacha tabia ya kuchezea vitu mdomoni ambavyo vinaweza kuleta madhara kwakuwa kitu hicho kikingia kwenye mfumo wa hewa kinaweza kusababisha madhara mbalimbali.