NA TERESIA MHAGAMA,DAR ES SALAAM

kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Misri
ukiongozwa na Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa nchi
hiyo, Assem Elgazzar katika kikao kilicholenga maendeleo ya mradi
wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kilichofanyika jijini leo Januari
21, 2023 Dar es Salaam.

akizungumza na ujumbe kutoka Misri ukiongozwa na Waziri wa Nyumba,
Nishati na Maendeleo ya Makazi wa nchi hiyo, Assem Elgazzar( hawapo pichani)
katika kikao kilicholenga maendeleo ya mradi wa umeme wa Julius
Nyerere (JNHPP) kilichofanyika jijini leo Januari 21, 2024 Dar es salaam
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Nishati na
Maendeleo ya Makazi wa Misri, Assem Elgazzar ambapo kikao hicho
kilijikita kuzungumzia maendeleo ya mradi wa umeme wa Julius Nyerere
(JNHPP) ambao kwa sasa umefikia asilimia 95.83.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Januari 21 , 2024 jijini Dar es
Salaam, ambapo Waziri wa Misri aliongozana na watendaji wakuu wa
kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors (wanaotekeleza mradi wa
JNHPP) na kwa upande wa Tanzania, viongozi waliohudhuria ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi
Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.
Dk.Biteko ameeleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na
Wakandarasi pamoja na TANESCO huku akieleza kufurahishwa kwake na
taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa kampuni ya Elsewedy, Eng.
Wael Hamdy ya kuwa majaribio ya mtambo namba tisa katika mradi wa JNHPP
yameleta mafanikio na kilowati 100 zimeanza kuingizwa gridi ya Taifa.
“Kikao hiki kimejikita kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu mradi wa
JNHPP, Mhe. Waziri Elgazzar ametumwa na Rais wa Misri kwa ajili ya
kuona maendeleo ya mradi huu, jambo lilitofurahisha hapa ni majaribio
ya mtambo namba Tisa yanaendelea na kwa hatua ya mwanzo ambayo
wamejaribu kuzungusha mtambo kwa njia ya maji wamefanikiwa kwa kiasi
kikubwa na wameingiza kilowati 100 kwenye gridi ya Taifa.” amesema
Dk. Biteko
Ameeleza kuwa, mafanikio ya majaribio hayo yanaleta matumaini kwani
ratiba ya kazi inaenda mapema zaidi ya iliyopangwa mwanzo na hii ni
kutokana na kazi nzuri ya Wakandarasi pamoja na TANESCO na kwamba
lengo ni kuzalisha megawati 235 kutoka mtambo namba 9 ifikapo Februari
mwaka huu na kuendelea na mitambo mingine ikiwemo mtambo Namba 8 na
Namba 7.
Ameongeza kuwa, mradi huo ni wa kipaumbele cha Rais, Dk. Samia Suluhu
Hassan ili watanzania wapate umeme wa uhakika kwa kuwa mradi huo
ukimalizika utaingiza megawati 2115 katika gridi ya Taifa.
Amesema kuwa, katika kikao hicho wamezungumza pia kuhusu masuala fedha
zilizotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii zinazotokana na uwepo wa
mradi huo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya mkataba.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko ameomba Watanzania wawe na subira
wakati Serikali ikitekeleza miradi mbalimbali itakayoongeza kiasi cha
umeme nchini ikiwemo mradi huo wa JNHPP.
Vilevile amesema kuwa, mradi wa JNHPP ni wa kielelezo kwa Afrika kwani
inaonesha kuwa nchi za Kiafrika zinaweza zenyewe kutekeleza miradi
mikubwa ya kimkakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa
Misri, Elgazzar amesema kuwa nia ya Serikali hiyo kutoka
mwanzo ni kuona kuwa mradi huo unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati
na amewapongeza wakandarasi pamoja na TANESCO kwa hatua nzuri ya
utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kuwa, Serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwapa ushirikiano
Wakandarasi hao katika hatua zote za utekelezaji wa mradi na kueleza
kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa kampuni za nchi hizo
kuendelea kuaminika kwenye utekelezaji wa miradi mingie ikiwemo ya
umeme.