NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imesema,akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha ikiwa ni takribani Dola Bilioni 5 kwa mwezi Novemba 2023, kiasi kinachotosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi kinachozidi miezi minne.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba
Taarifa hiyo ilieleza kuwa hayo yalibainika baada ya kamati hiyo kufanya kikao chake cha 229 juzi , kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi.
Vile vile taarifa hiyo ilifafanua kuwa,thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani iliipungua kwa asilimia 7.8 kwa mwaka, hali inayoakisi upungufu wa fedha za kigeni nchini.
“Hata hivyo, akiba ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha,”alifafanua taarifa yqma Mwenyekiti huyo.
Aidha, Sekta ya fedha iliendelea kuwa thabiti. Sekta ya benki ilibaki imara ikiwa na mitaji ya kutosha na ubora wa rasilimali za benki ukiongezeka, kiwango cha mikopo chechefu kilipungua kufikia asilimia 5.3 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.2 mwezi Oktoba 2022.
“Kamati ya Sera ya fedha iliridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kukabiliana na uhaba wa fedha za kigeni nchini.
“Vilevile, utekelezaji wa sera zenye lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, unatarajiwa kuimarisha urari wa bidhaa, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, kuongeza akiba ya fedha za kigeni na hivyo kupelekea utulivu wa thamani ya Shilingi.”
Kamati pia ilipongeza jitihada zilizochukuliwa na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya programu mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwa ni pamoja na yale yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF ya Extended Credit Facility (ECF).
Wakati huo huo taarifa hiyo ilieleza kuwa, Kamati ilibaini na kupongeza hatua zillizofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kuhamia kwenye mfumo mpya wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha utakaoanza Januari 2024.