NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
DESEMBA 15 Mwaka huu , Tume ya Tehama (ICTC) ilisaini hati ya makubaliano na ushirikiano na Taasisi ya Ruge Mutahaba ya kuinua vijana na wanawake waweze kushiriki na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Makubaliano hayo yamelenga kushughulikia maeneo ya utafiti, ukuzaji ujuzi na ubunifu kupitia mafunzo, warsha na mikutano.
Makubaliano hayo yalisainiwa ya Dk Nkundwe Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC kwa niaba ya Tume na Cynthia Bavo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ruge Mutahaba katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Dk.Mwasaga alisema ICTC imefikia makubaliano kwa lengo la kuwawezesha makundi hayo kuwa na uwezo wa kuchangamkia fursa zilizopo katika Uchumi wa Kidigitali.
Alisema Tume ipo tayari kutekeleza jukumu walilokubaliana na taasisi ya Ruge Mutahaba kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Tehama na sera nyingine zinazoitegemea TEHAMA kama nyenzo kuu ya kufikia malengo ya sera husika.
“Kwa hiyo tumeona tuongeze nguvu ya ushirikiano katika kuwainua kisekta wanawake na vijana katika maeneo ya utafiti, ubunifu, na kuwajengea ujuzi na uwezo kwa ujumla kwa njia mbalimbali…uchumi wa dunia unakwenda kushikwa na sekta ya tehama hivyo ni vyema wanawake na vijana wakaandaliwa vyema katika eneo husika, kuanzia ubunifu, utafiti na kadhalika,” alisema Dk.Mwasaga.
Naye Bavo ambaye taasisi yake ilianzishwa Juni 22, 2022 kwa lengo la kuendeleza maono ya Ruge Mutahaba ambaye enzi za uhai wake alijikita zaidi katika ustawi wa vijana, wanawake watanzania kwa ujumla, alisema wana kila sababu ya kuendeleza mazuri ya Ruge.
Taasisi ya Ruge imejikita katika dhima kuu tano ambazo ni ubunifu, uvumbuzi, umahiri, upambanaji na uzalendo, na ili kutekeleza hayo, inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, sekta binafsi na mashirika ya ndani na ya Kimataifa katika kuendesha miradi ili kutatua changamoto za wanawake na vijana hasa katika eneo la ajira na kutengeneza kipato.
“Enzi za uhai wake, Ruge aliwekeza sana katika ubunifu na ujasiriamali wa vijana na wanawake ili kuwasaidia katika kuinua kipato…hivyo tunalenga kuyapa uhai na kutekeleza maono yake chanya ya kimaendeleo yaliyolenga vijana na wanawake kwa kupitia fursa mbalimbali,” alisema na kusisitiza kuwa, taasisi ina mikakati ya kuendesha miradi ya kusaidia wanawake na vijana kupitia ujasiriamali wenye tija, sanaa na ubunifu.
Mbali na ushirikiano na Taasisi ya Ruge Mutahaba, katika kujenga uwezo na kukuza taaluma ya Tehama nchini, Tume ya Tehama katika mwaka huu wa fedha imejipanga katika kuendelea na ukamilishaji wa vituo vya ubunifu TEHAMA (Soft centers) katika Kanda 5 pamoja na kuanzisha kituo kimoja Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dk. Mwasaga,Tume pia inalenga kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya Tehama kuwezesha uanzishaji wa vituo vya majaribio vya ubunifu Tehama katika ngazi za wilaya, kufanya tafiti za maendeleo yake na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Tehama
Tume pia inalenga kuratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za Tehama ndani na nje ya nchi, kushirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za Tehama ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za Tehama hapa nchini, kujenga kujenga kituo cha Akili Bandia na kuanzisha Kituo cha Resilience Academy hapa nchini kwa ajili ya kuendeleza wataalamu wa Tehama
Imelenga pia kuwezesha mafunzo maalumu ya wataalamu wa Tehama 500, kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogondogo ‘startup’ kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za ‘startups ‘duniani, na kadhalika.
Hivi karibuni, Tume ilipeleka wabunifu saba katika maonesho ya Afrika yaliyofanyika Algiers, Algeria kwa lengo la kuwakutanisha na wabunifu na wawekezaji mitaji wa kimataifa ikiwa na matarajio ya kuongeza fursa kwa kampuni changa za Tehama kupanua na kukuza mitaji yao ya kibiashara.
Pamoja na mambo yote mazuri yaliyo katika makubaliano baina ya ICTC na Taasisi ya Ruge Mutahaba nihitimishe kwa kuzipongeza Taasisi hizo mbili na kuzitaka kuyaenzi makubaliano hayo kwa kuongeza fursa kwa ajili ya kumuenzi zaidi aliyekuwa na ndoto za kuwakwamua zaidi vijana wa kike na kiume ili kufikia malengo kusudiwa.