NA MUNIR SHEMWETA, WANMM, SINGIDA
WANANCHI wa Mwankoko Manispaa ya Singida wametakiwa kuridhia fidia waliyopewa ili kupisha eneo la chanzo cha maji kinachotumika na wakazi wa mji wa Singida.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa leo Oktoba 10 , 2023 alipotembelea mradi wa chanzo cha maji cha Mwankoko wakati akifuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiii 975.
Katika chanzo hicho cha maji, wananchi wa eneo hilo wamekuwa na malalmiko ya muda mrefu ya madai ya fidia kutokana na maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya kupisha chanzo cha maji kinachotumika na wakazi wa mji wa singida.
Awali katika kumaliza changamoto hiyo wananchi hao walitakiwa kuwasilisha malalamiko kwa maandishi na mthamini mkuu wa serikali apitie utaratibu mzima wa zoezi la uthamini ili kubaini changamoto na kutoa majibu ambapo baada ya kupitia malalamiko hayo ofisi hiyo ya mthamini ilijiridhisha kuwa wananchi hawakuwa na madai ya msingi na kuwataarifu kwa barua ya sept 18, 2023.
Akiwa eneo la chanzo hicho cha maji cha Mwankoko, Waziri wa Ardhi Silaa alielezwa na Diwwani wa Mwankoko Emanuel Emadaki kuwa, utata wa madai ya fidia kupisha kupisha chanzo cha maji cha Mwankoko unatokana na sitomfahamu ya kujua kiwango halisi cha fidia anayotakiwa kulipwa mwananchi anayepisha mradi wa chanzo cha maji.
“Utata umeanza baada ya wananchi kutofahamu bei elekezi ya maeneo yao kwa kuwa ardhi shamba ingeonesha tofauti na ardhi isiyolimwa sasa hiyo changamoto pamoja na wananchi kulipwa fidia lakini walikuwa wakisubiri bei elekezi” alisema diwani wa Mwankonko Emadaki
Kwa upande wake Waziri Silaa amesema, baada ya kupata maelezo kutoka mamlaka husika amejiridhisha pasipo shaka kuwa, wananchi wanaolalamika wamelipwa fidia stahiki na ndiyo maana hata baadhi ya wachache wao walioemda mahakamani walishindwa kesi.
Amewaomba viongozi wa Mwankoko kwenda kuwaeleza wananchi kuwa, suala hilo liimefika mwisho na mogogoro wao siyo tu umetatuliwa katika ngazi ya wilaya au mkoa bali umefika katika hatua Baraza la Mawaziri jambo linaloonesha serikali yao chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyowajali kwa kuwa mgogoro wa watu 215 umefika Baraza la Mawaziri.
“Leo nimefika kufuatilia migogoro minne hapa singida na kati ya hiyo huu hapa nao umo sasa nisiondoke singida nikuambie wewe mwenyekiti ukawaambie mgogoro umefika mwisho ni vyema wakubali na kama wana nia nyingine nje ya mgogoro kwa muda wao waende ofisi ya kamishna” amesema.