NA MUNIR SHEMWETA,WANNM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maedeleo ya Makazi Jerry Silaa ametoa siku saba kupatikana suluhu ya changamoto za urasimishaji makazi holela wa makazi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Agizo la Waziri Silaa linafuatia mkoa wa Dar es Salaam kuwa moja ya mikoa yenye malalamiko mengi ya urasimishaji makazi holela zoezi ambalo lilianza mwaka 2013 na kutarajiwa kukamilika mwaka huu 2023
Silaa ametoa agizo hilo Oktoba 4, 2023 alipokutana na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na watendaji wa sekta ya ardhi kujadili utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa upande wa sekta ya ardhi.
” kero ni kubwa nikitoka hapa naenda kukaa na wenzangu wizarani ili zoezi hili katika mkoa wa Dar es Salaam lifanyike haraka na lifike mwisho” alisema Silaa.
Amesema, pamoja na hatua iliyofikiwa kwenye urasimishaji, utekelezaji wa programu hiyo umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo makampuni yaliyopewa kazi hiyo kushindwa kukamilisha kwa wakati huku wananchi wakikosa imani kwa makampuni na kuacha kuhangia gharama za utekelezaji kazi hiyo na kusababisha zoezi hilo kukwama katika maeneo mengi.
Waziri Silaa ameeleza kuwa, kama kuna makampuni yamefanya vibaya katika zoezi la urasimishaji basi yapewe adhabu zake na wananchi wajue na iwapo kuna makampunii kazi zo zimekwama basi zikwamuliwe na kama kuna wananchi waliokwama kupata hati basi wapatiwe.
Amesema, athari za zoezi hilo la urasimishaji kwa mkoa wa Dar es Salaam ni kubwa sana ukilinganishwa na mikoa mingine huku akibainisha kuwa jumla ya vipande vya ardhi vilivyotambuliwa ni 625,639 kati ya hivyo upangaji umekamilika kwa viwanja 556,755 ilihali upimaji ukiwa umefanyika kwa viwanja 125,035 na umilikishaji ukiwa viwanja 28,902 pekee.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, Rais Dk Samia Suluhu Hassan amemteua na kumuamini afanye kazi ya ardhi na yeye ameamua kufanya hivyo ili kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kero za ardhi nchini.
“Mimi naamini kwa kero za dar es salaam na umuhimu wa mkoa huu tuache mengine yote na tutafute suluhu ya urasimishaji kwa mkoa wa dar es salaam” alisema
Vile vile, Waziri Silaa ameongeza kuwa, katika kuhakikisha wizara yake inaondoa kero za ardhi nchini wamejipanga kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kusogeza huduma karibu na wananchi.
Ametaja baadhi ya hatua za usogezaji huduma kwa wananchi kuwa, ni kuwa na ofisi za ardhi kwa kila mkoa zikioongozwa na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa tofauti na huko nyuma ambapo huduma zilikuwa zikitolewa kwenye ofisi za kanda.
Aidha, amesema kwa ile mikoa yenye changamoto kubwa kama Dar es Salaam wameweka makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa wawili lengo likiwa kurahisisha utendaji kazi.
Hata hivyo, amesema wizara yake inafikiria kuwa na mpango wa ikiwezekana kuwa na mikoa maalum ya ardhi katika wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam.
” ukiangalia takwimu za mahitaji ya hati mkoa kama katavi unatoa hati 850 kwa mwaka na mkoa wa Dar es salaam unatoa hati 16000 kwa mwaka hivyo utaona wingi wa mahitaji ya hati kwa wananchi wetu” alisema