NA DANSON KAIJAGE, DODOMA
WATANZANIA wenye uwezo wa kifedha wametakiwa kuwekeza miradi mikubwa ya kimaendeleo badala ya kufikiria kuwekeza nje ya nchi.
Hayo yameelezwa Oktoba 3, 2023 na Isaack Piganio ambaye ni Meneja wa kampuni ya Mati Super Brand Limited,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa wazawa kuwekeza nchini muda mfupi baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili katika viwanja vya shule ya msingi Chamwino jijini Dodoma.
Piganio amesema kuwa kitendo cha wazawa kuweka uwekezaji wa miradi ya maendeleo nchini ni sehemu ya kuchochea suala zima la uzalendo na kuongeza ajira kwa watanzania sambamba na pato la mtu mmoja mmoja.
Akizungumzia kampuni hiyo amesema kuwa chimbuko yake ni mkoani Manyara na kueleza kuwa wameamua kuzunguka na Mwenge kwa ajili ya kuonesha uzalendo wa kutangaza bidhaa ambazo zinazalishwa na kampuni hiyo ambazo kwa asilimia kubwa malighafi inapatikana nchini.
Sambamba na hilo amesema ili kuonesha uzalendo kama ni lazima kutengeneza bidhaa ambazo ni bora na zinazoweza kuingia katika ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi kwa maana ya soko la kimataifa.
“Napenda kuwaambia watanzania wenzangu ambao wana uwezo wa kufanya uwekezaji wakawekeza ndani ya nchi kwa kutambua kuwa uwekezaji huo utawasaidia vijana wa kitanzania kupata ajira kadri ya uwezo wa mtu alionao.
“Kama hiyo haitoshi iwapo wawekezaji wazawa watawekeza nchini watasaidia mzunguko kuwa mkubwa nchini kuwa mkubwa na wakati mwingine kupata fedha za kigeni pale ambapo watauza bidhaa zao kwa masoko ya kimataifa”ameeleza Brand Meneja wa kampuni ya Mati Super Brand limited .