NA WMJJWM MAGU, MWANZA
WANANCHI wilayani Magu mkoani Mwanza wamehamasika katika zoezi la kuboresha makazi yao na kujenga nyumba 165 kwenye Kata Nne Wilayani humo.
Hayo yamebainika katika ziara ya Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sera na Afua mbalimbali za maendeleo na Ustawi wa Jamii Septemba 16, 2023 wilayani Magu mkoani Mwanza
Akitoa taarifa ya Kampeni ya Makazi Bora Wilayani humo Mkurugenzi wa Kivulini Yasin Ali amesema Shirika hilo limefanikiwa kuhamasisha Jamii kuboresha makazi yao kwa kutumia vikundi vya umoja ikiwemo Wanawake na mashabiki wa Timu za mpira wa Miguu.
“Mhe. Naibu Waziri tumefanikiwa kuhamasisha wananchi kuachana na nyumba za nyasi na kujenga nyumba za Bora za bati na tumekuja na namna ya kipekee ya kuhamasisha Jamii kwa kuhusisha mashabiki wa Timu za mpira za Simba na Yanga ili waungane kwa pamoja kusaidiana kuboresha makazi yao ” alisema Yasin
Yasini amesema, Shirika la Kivulini limehamasisha makazi Bora na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto katika Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Mara, Geita na Shinyanga.
Akizungumza na wananchi katika eneo hilo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara inafanya Kampeni ya Makazi Bora kwa Mikoa mbalimbali kwa ushirikiano na Mikoa na Halmashauri ambapo kuanzia Julai 2022 hadi Aprili 2023 jumla ya nyongeza ya nyumba 732 zilijengwa kwa hamasa ya Kampeni hiyo na kufikisha jumla ya nyumba 5712.
Amesema kuwa maendeleo endelevu yanatokana na wananchi wenyewe hivyo ameihasa Jamii kuongeza juhudi kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo Kampeni ya Taifa ya ujenzi wa Makazi bora na kukuza Moyo wa uzalendo katika kufanya kazi kwa bidii.
“Katika ziara yangu nimetembelea nyumba ya Mama aliyenyanyasika na Mumewe na kuachwa na Watoto ila hakuwa mnyonge akapambana na sasa ameshaanza kujenga nyumba bora ili watoto wake waishi kwenye hali nzuri”alieleza Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amepongeza juhudi za Shirika Lisilo la Kiserikali la Kivulini kwa kuhamasisha Jamii na kutoa elimu ya kupinga ukatili, malezi na Makuzi na kuboresha makazi ndani ya jamii kwa Mikoa mbalimbali nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kasanda amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameshirikiana na Serikali kufanya kazi kubwa ya kuingia kwenye Jamii kwa kutoa elimu na kutatua changamoto kadhaa ikiwemo kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Nao baadhi ya wananchi katika eneo hilo wameishukuru Serikali kwa kuunganisha nguvu za pamoja na wadau kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuhamasisha Jamii katika kuboresha makazi yao.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makao ya Watoto ya Main Springs yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu na amewaasa wamiliki wa Makao ya Watoto nchini kuendesha Makao kwa kuzingatia Sheria, taratibu, mila na desturi za kitanzania.