NA MWANDISHI WETU, MBEYA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vyema kuimarisha ulinzi na usalama kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Mbarali.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 18, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amesema, “Vikosi vyote vya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya vipo imara na vipo kazini kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa maeneo yote ya Wilaya ya Mbarali” alisema Kamanda Kuzaga.
Aidha, Kamanda Kuzaga amewataka wananchi wenye sifa na vigezo vya kupiga kura kwenda kwenye vituo vya kupigia kura ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kumchagua mbunge wa jimbo lao bila hofu yoyote kwani ulinzi na usalama ni wa kutosha.
Jumla ya vyama vya siasa nane vinashiriki uchaguzi huo ambavyo ni CCM, ADC, UPDP, DP, NLD, UDP, TLP na ACT WAZALENDO.
Uchaguzi huu unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mbarali kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Francis Mtega kufariki dunia baada ya kugongwa na Trekta Power Tiller Julai mosi 2023 huko wilayani Mbarali.
Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Mbarali utafanyika leo Jumanne Septemba 19, 2023