NA MWANDISHI WETU, TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga . Waziri Kindamba amesema mchezo wa fainali ya Kombe la shirikisho la Azam (ASFC) uliochezwa Juni 12, 2023, kati ya Timu ya Yanga SC na Azam FC, katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga,unatarajiwa kutoa fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Jiji la Tanga kutokana na idadi kubwa ya wageni waliofika kuangalia mchezo huo.
Kindamba ameyasema hayo ofisini kwake alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiongozwa na Rais wa TFF, Wallace Karia, waliofika ofisini kwake kumsalimia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa fainali ya ASFC unaochezwa leo Jijini hapa.
Amesema ni faraja kubwa kwa fainali hiyo kuchezwa katika uwanja wa Mkwakwani, na kwamba Serikali ya Mkoa imetoa baraka zote kufanyika kwa mchezo huo huku akiwahakikishia usalama wa watu na mali zao kabla, wakati na baada ya mchezo.
Aidha amewataka wageni wote kufurahia mchezo huo na kujiepusha na matendo ya jinai.
Kwa upande wake Rais wa TFF Wallace Karia amesifu jitihada kubwa za uboreshaji wa Uwanja wa Mkwakwani ambapo amesema kwa sasa upo kwenye ubora wa hali ya juu.
Karia amesema fainali ya leo itaenda pamoja na tukio la utoaji wa tuzo mbalimbali litakalo fanyika usiku wa leo katika kituo cha Michezo cha Mnyanjani, ambapo kutakuwa na tuzo kwa wachezaji mbalimbali na tuzo za heshima.