NA DENIS CHAMBI, TANGA
JUMLA ya miradi 92 ya maendeleo iliyotekelezwa katika mkoa wa Tanga iliyogharimu zaidi ya Sh. Billioni 27 inatarajiwa kuzinduliwa , kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi na mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023.
Akipokea mwenge wa Uhuru kitaifa leo Juni 9 , 2023 katibu tawala mkoa wa Tanga Pilli Mnyema katika uwanja wa ndege ukitokea mkoa wa Kusini Pemba alisema kuwa miradi yote hiyo imetokana na nguvu za wananchi fedha kutokana serikali kuu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
“Mwenge wa Uhuru tuliokabidhiwa leo hii utakimbizwa katika halmashauri 11 na wilaya zake 8 za mkoa wa Tanga zenye umbali wa Kilomita 1959 na kufungua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi jumla ya miradi ya maendeleo 92 yenye thamani ya shilingi za kitanzania Bilioni 27, 419, 792, 394.01”
“Mchanganuo wa fedha hizo ni nguvu za wananchi Billion 1.8 Halmashauri za wilaya , Bilioni 1.97, serikali kuu billion 13.06, wadau wa maendeleo na sekta binafsi billioni 10.58 tunashukuru sana Rais Samia kwaajili ya kuwezesha fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi hii, miradi yote hii imefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya serikali nguvu za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo ” amesema Mnyema.
Amesema mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2022 ndani ya mkoa wa Tanga wenye wilaya 8 na Halmashauri 11 jumla ya miradi 82 ilizinduliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa ambayo ulikuwa na miradi Bilioni 33.39 ambayo hadi sasa kwa asilimia kubwa imekamilika na mingine inaendelea.
Katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu kwa vitendo ambayo inasema tunza mazingira okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe na uchumi wa Taifa mkoa wa Tanga umeadhimia kupanda miti millioni moja kila eneo na tayari kwa mwaka huu wa 2023 zaidi ya 7, 000 sambamba na kuhakikisha wanaendelea kuimarisha ulinzi katika vyanzo vya maji vilivyopo.
“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu tunaendelea kuhakikisha halmashauri zote zinatekeleza agizo la kupanda miti kwa vitendo na kwa takwimu tulizonazo kwa mwaka huu 2023 tumepanda miti takribani 7,35,903.5” ameongeza Katibu Tawala huyo.
Aidha ameongeza kuwa katika kusimamia katazo la matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari jumla ya kilogramu 838.8 ya vifungashio visivyoruhusiwa kisheria vimekusanywa na kuhifadhiwa kwaajili ya taratibu zingine.
“Tumeendelea kufanya operesheni ya katazo la mifuko ya plastiki na vifungashio ambavyo hairuhusiwi kisheria na wananchi wameendelea kupewa elimu ikiwemo mikitano ya vijiji na halmashauri, na hadi kufikia Mei 30, 2023 jumla ya kilogram 838.8 ya vifungashio visivyoruhusiwa kisheria vimekusanywa kwaajili ya kuendelea na taratibu nyingine” amesema
Katibu tawala huyo ameeleza kuwa katika miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita mkoa wa Tanga umepokea jumla ya shilingi Trilion 2.26 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu , afya na barabara.
“Katika miaka miwili ya serikali ya miaka miwili ya Dk Samia Suluhu Hassan mkoa wetu wa Tanga imefanikiwa kupokea fedha jumla ya shilingi Trilioni 2.126 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mfano katika sekta ya elimu mkoa wetu umepokea zaidi ya shilingi Bilioni 137.3 kwenye afya umepokea jumla ya shilingi Bilioni 80.5 na sekta ya maji Bilioni 1.2”