NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MDHAMINI Mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) leo Juni 9, 2023 imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa timu ya Yanga ambayo ndiyo bingwa kwa msimu wa 2022/2023.
Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa ilifanyika katika uwanja wa Kumbu kumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku ikishuhudiwa na mamia ya wapenda soko wakazi wa jiji hilo na meneo ya jirani baada ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Tanzania Prison.
Akikabidhi kombe hilo kwa Yanga mkuu nwa mkoa wa Mbeya Juma Homera aliishukuru benki ya NBC kuwa mdhamini mkuu wa ligi kuu ya Tanzania bara na kusema kuwa udhamini wa NBC umekuwa na matokeo chanya kwa soka la Tanzania.
“Udhamini wa NBC umewezesha kuongeza ushindani kwenye ligi na kuboresha soka letu. Leo hii tunajivunia kuwa na ligi bora barani Afrika tukishikilia nafasi ya tano.
” Naipongeza sana benki ya NBC kwa kufanya mambo makubwa katika ligi na soka la nchi yetu kwa ujumla,” amesema Homera.
Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa na kusema kuwa haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuibuka kinara wa ligi kutokana na ushindani mkali kutoka kwa timu pinzani.
Kwa upande wake mkurugenzi wa fedha wa NBC Barnabas Waziri alisema NBC itaendelea kuwa mdhamini mkuu wa ligi na kuongeza kuwa benki hiyo pia itaendelea kutoa mchango katika sekta ya michezo kwa upana wake.
“Pamoja na soka, tumekuwa tukisadia michezo mingine kama riadha kupitia NBC Dodoma marathon. Nia yetu ya kusaidia sekta ya michezo hapa nchini ni thabiti na tutaendelea kusaidia,” ameeleza
Mkurugenzi huyo amesema udhamini wa NBC kwenye ligi kuu umekuja na maboresho kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa bima kwa wachezaji wa ligi kuu pamoja na familia zao pamoja na mikopo ya mabasi kwa vilabu vinavyoshiriki ligi.
“Juzi tumezindua kombe jipya lenye hadhi na ambalo leo litakabidhiwa kwa bingwa wa ligi. Ili kuongeza hamasa kwa wachezaji na makocha, tumekua tukitoa tuzo mbali mbali kwa makocha na wachezaji bora wa mwezi,” amesema
Mkurugenzi huyo aliipongeza Timu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo na pia alizipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi ambayo ushindane wake umekuwa ni mkubwa.