NA DENIS SINKONDE, SONGWE
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania (TFS )wilaya ya Ileje mkoani Songwe imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya masoko ya Mbangala na Sange Kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200 pamoja na kulipa fidia Kwa wananchi.
Kaimu Mhifadhi Mkuu ,shamba la miti Lyondo Mswima Emanuel alisema wakala wa huduma za misitu kwa kushirikiana na mamlaka za uthaminishaji imelipa fidia kwa wamiliki wa vibanda vya biashara 61 shilingi milioni 55,716,083 na kaya 11 umelipa shilingi milioni 67,355,151.
Amesema TFS imefanikiwa kujenga miundombinu kwenye masoko mawili ambayo yamejengwa kama mbadala wa soko la Katengele ambapo soko la Mbangala shilingi milioni 49,457,550 na soko la Sange jumla ya shilingi milioni 49,457,550 zimetumika kukamilisha miundombinu hiyo.
“Masoko hayo mawili yamejengwa ikiwa ni mbadala wa soko la Katengele ambapo Halmashauri wameshirikiana vyema na TFS kuhakikisha shamba la miti Iyondo Mswima linabaki salama bila kuvamiwa,”amesema Emanuel.
Kukamilika Kwa miundombinu hiyo kumepelekea mkuu wa wilaya hiyo Farida Mgomi kuzungumza na wafanyabiashara hao kuwataka kuhamia kwenye masoko hayo kufikia Juni 24 ,2023.
“Kwenye masoko hayo tumefanikiwa kujenga Banio la mifugo, Machinjio, choo na vituo vya maji ambapo jumla ya shilingi milioni 98,915,100 zimetumika kama gharama ya ujenzi wa miundombinu hiyi”, amesema
Mgomi alisema kukamilika Kwa masoko hayo ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassani alilolitoa Julai 24, 2018 akiwa Makamu wa Rais alipofanya mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Sange.
Mgomi alisema kuhamishwa Kwa wananchi na soko la Katengele ni mpango wa Serikali kuendeleza shamba la miti Iyondo Mswima lenye jumla ya Hekta 5418 ambapo no uhifadhi wa miti ya asili na upandaji wa miti ya kigeni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ileje Ubatizo Songa alieema kukamilika Kwa miundombinu ya masoko hayo kutapelekea wananchi kupanga siku tofauti za kufanya biashara zao ili wajiingizie kipato.
Akizungumza kwaniaba ya wananchi waliofika kwenye soko hilo Joseph Msokwa aliipongeza serikali kwa maamuzi ya kujenga miundombinu ya masoko mengine na kulipa fidia Kwa wathirika hivyo agizo la kuhama eneo hilo wanalipokea ili kuanza maeneo mapya walikohamishiwa kufikia Juni 24 mwaka huu