NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya ameieambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba wanasubiri majibu ya barua waliyomuandikia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuhusiana na kukiri na kuomba kupunguziwa adhabu
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh.Bilioni 5.1 kwa njia ya udanganyifu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kumuuliza Wakili wa utetezi anayemuakilisha Gasaya, Nafikire Mwambona wamefikia hatua gani kuhusiana na mshtakiwa huyo kuandika barua ya kukiri kosa linalowakabili.
Ndipo Wakili wa utetezi Mwambona alimjibu kuwa wamejaribu kufuatilia lakini wameelezwa kuwa anayehusika na kujibu barua hiyo hayupo hivyo wanaendelea wanaendelea kusubili ili barua yao iweze kujibiwa.
“Tumejaribu kufuatilia tunasubili tujibiwe barua yetu tuliyoileta kwa DPP na tumesikia kuwa kiongozi wao anayeshughulikia barua za kukiri hayupo lakini tumeambiwa hadi wiki ijayo atakuwa amerudi,”amedai Mwambona.
Awali Wakili wa Serikali, Frenky Michael alieleza Mahakama hiyo kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo wanasubili majibu kutoka kwa DPP iweze kumjibu.
Hakimu Kabate aliahirisha shauri hilo hadi Juni 6, 2023 kwa ajili ya kutajwa na kuonana na kiongozi wa waendesha mashtaka wa mahakama hiyo ili wapewe majibu kutoka Kwa DPP.
Mshtakiwa huyo yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.