DENIS CHAMBI, TANGA
MKUU wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amewatahadharisha watumishi wote ndani ya mkoa huo kutokujihusisha na aina yeyote ya makundi ikiwemo ya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo wanakwenda kinyume na taratibu kanuni na sheria zinazowaongoza.
Akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza wakati akimalizia ziara yake kwa mkoa nzima kuzungumza nao pamoja na madiwani zikiwemo kamati za fedha Kindamba amewataka kudumisha umoja, amani na mshikamano baina yao na kila mmoja kuisimamia na kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi.
“Haiwezekani sisi watumishi tukajiingiza katika makundi haiwezekani kabisa, niwatake watumishi wenzangu wa Muheza kitu hicho tuache kinakwamisha mambo mengi sana , nimemuagiza mkurugenzi fannya utafiti wako watu wanaojikusanya kwenye makundi walete tutawatoa hapa Muheza tafadhali sana watumikie wananchi”
“Mtumishi umekuja kufanya kazi hapa sio kujiingiza katika siasa hazikuhusu achana nazo, fanya lililokuleta wacha kujiingiza kwenye makundi na sisi hatutacheka na mtu anayejiingiza kwenye kikundi cha wana siasa wa maeneo husika iwe Muheza, Kilindi Pangani au kokote kule tukishakujua wewe ni mtumishi unajiingiza kwenye makundi tutakushughulikia”
” Pamoja na yote nawaombeni sana mdumishe umoja mshikamano na kushirikiana, umoja kwa madiwani na watumishi wenyewe, haiwezekani menejimenti inagawanyika kuna anayemuunga mkono mkurugenzi wa sasa na aliyepita hapana! acheni kabisa hatuwezi kutoka kwa namna hiyo migawanyiko hiyo haifai, yaliyopita si ndwele tugange yajayo wakati wangu mimi sitakubali na kuruhusu mivutano” amesema Kindamba.
Sanjari na hayo amewataka watumishi hao pamoja na madiwani kwa ujumla kuhakikisha wanafanya matumizi ya fedha kwa kadiri zilivyopangwa katika miradi husika na kuisimamia kuhakikisha inakamilika kwa wakati na weledi wa hali ya juu na sii vinginevyo.
“Fedha zinazoletwa zinachelewa kutumika, mkoa huu hauna historia njema sana na matumizi ya fedha za serikali haiwezekani fedha zinaletwa nmarumbana kuzitumia mpaka zinapelekwa mkoa mwingine, sitaki mvutano wa aina yeyote wakati wangu mimi ninahitaji maneno kidogo vitendo vingi na tukikubaliana twendeni tukatekeleze tulichokubaliana” ameongeza Kindamba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza Erasto Mhina akizungumza kwa niaba ya baraza la madiwani na watumishi alisema kuwa wataendelea kuisimamia miradi iliyoelekezwa kutekeleza miradi ndani ya wilaya hiyo pamoja na kuwasimamia watendaji wote kwa mustakabali nzima wa maendeleo ya wananchi sambamba na kuboresha utoaji huduma.
“Kwa niaba ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza yale yote uliyoyasema tumeyasikiliza kwa makini sana na yale ambayo yalikuwa yanaonekana kama makando kando ya wilaya ya Muheza nikuhakikishie kabisa kwamba tumeyamaliza na tunasonga mbele sasa na maneno yako yote tutayafanyia kazi” amesema Mhina.
Amesema Muheza wana rasilimali nyingi ambazo zinaweza kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje watakaokuja kuwekeza na hatimaye kuwaletea maendeleo pamoja na chanzo cha ajira ikiwemo machungwa yanayozalishwa kwa wingi bila ya kusahau uwepo wa madini hivyo kumuomba mkuu wa mkoa kuwasaidia kupatikana kwa wawekezaji.
” Wilaya ya Muheza tuna fursa nyingi ukiangalia matunda , ukienda kwenye viungo lakini pia na madini lakini kama haitoshi tuna mawe ambayo yanaweza kuwa bidhaa na kutengeneza uchumi mkubwa kama ilivyo Chalinze ukituunga mkono kutupatia wawekezaji utakuwa umetusaidia sana lakini pia ukipata mwekezaji ambaye tunaweza kushirikiana naye sisi tuko tayari” ameongeza Mwenyekiti huyo