NA BARAKA JUMA , MWANZA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limemtunuku cheti cha shukrani mwandishi wa Habari wa gazeti la Uhuru,Baltazar Mashaka kutokana na kutambua mchango wake wa kuhabarisha jamii na umma wa waislamu.
Aidha baraza hilo pia liliwatunuku vyeti baadhi ya waandishi wa habari Soud Shaaban wa Star TV na Paulina David wa RFA.
Walitunukiwa vyeti hivyo jana Mei 17, 2023 na Mkuu wa Itifaki wa BAKWATA,Ustaadhi Twaha Utali kwa niaba ya Sheikh Hasani Kabeke,hafla iliyofanyika kwenye ofisi za BAKWATA mkoani Mwanza.
“Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipomshukuru (Baltazar Mashaka) kwa mchango wake kupitia kalamu,amekuwa mtu umuhimu, mahiri wa kuhabarisha na kuelimisha jamii wakiwemo waislamu mkoani humu na pengine nchini kwa taaluma yake,”
“Pia nampongeza na kumwombea heri Mwenyezi Mungu ampe afya na kumfanyia wepesi na wengine waige mfano wake,anajitoa mno katika shughuli za Baraza,”alisema Utali kwa niaba ya Sheikh Kabeke.
Kwa upande wake Mashaka aliishukuru BAKWATA kwa ushirikiano na kuahidi kutenda kwa weledi kuhakikisha jamii wakiwemo waislamu wanapata habari zenye maudhui bora ya kujenga,kuelimisha,kuburudisha na kukosoa bila upendeleo kwa mujibu wa taaluma.
“Naishukuru BAKWATA kwa kutambua mchango wangu na hii ni heshima kwangu na katika kumbukumbu kwa ujumla,naamini hata wengine watafanya vizuri na kutunukiwa heshima hii zaidi wakizingatia misingi ya taaluma yao kuhakikisha wanafikisha maudhui bora kwenye jamii,” alisema.