NA MWANDISHI WETU, KILINDI
MKUU wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amepiga marufuku uuzaji wa ardhi katika eneo lenye mgogoro wa wananchi kati ya vijiji vya Gitu na Ngobole wilayani Kilindi, mgogoro uliodumu kwa miaka 17 sasa.
“Naagiza na nasema marufuku kuendesha shughuli za kuuziana na uuzaji ardhi katika vijiji hivyo na ifikapo July 2023 nataka migogoro hii ya mipaka iwe umeshatatuliwa kikamilifu”.
Akizungumza akiwa katika eneo hilo mpakani hapo Kindamba amemtaka Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Gitu kusitisha kuuza maeneo yenye mgogoro hadi hapo Serikali itakapokuja na majibu ya utatuzi wa mgogoro huo.
“Nitoe onyo kwa yeyote atakaye jifanya mkaidi na kwenda kinyume na agizo langu awe Mwenyekiti wa Kijiji, wa Chama chochote au mkubwa yoyete kuwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yake na kwa hili sio kama natishia” amesisitiza Kindamba.
Aidha Kindamba amesema yapo mapendekezo yaliyotolewa na Kamishna wa Ardhi ambayo
sasa Mkoa pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (‘CCM’) ngazi ya mkoa tutapitia na kuyatekeleza mapendekezo ya Kamishina na hatimaye kuja na suluhisho la kudumu la mgogoro huo.
Amesema wananchi watakao fanya vitendo vya kuwashambulia watumishi wa Serikali wanapofika katika eneo hilo kwa upimaji wa mipaka vijijini humo kwamba atawashughulikia kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.
“Lengo ni kuutatua huu mgogoro, hivyo lazima mtoe ushirikiano kwa vyombo vyote vya Serikali vitakapokuja hapa, na sio kuleta mchezo wa kuwashambulia atakayefanya hivyo tutamnyakua sitaki mchezo wa kuzuia shughuli za maendeleo kwenye jambo hili” alisisitiza zaidi.
Awali akitoa taarifa juu ya mgogoro huo Ofisa Ardhi Wilaya ya Kilindi Natus Manumbu alisema vijiji hivyo viwili vinaitenganisha mikoa miwili ya Tanga na Manyara ambapo pia kuna mgogoro mwingine kati ya wakulima na wafugaji waliopo katika maeneo hayo.