NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania ( TanTrade) kwa kushirikiana na Baraza la Mchele Tanzania ( RCT) wametoa semina kuhusu upatikanaji wa masoko pamoja na taratibu za mauzo kwa wasindikaji na wafanyabiashara wa mchele katika eneo la Halmashauri ya Mbarali.
Washiriki wa Semina hiyo ni pamoja na viongozi waliowakilisha wafanyabiashara wa mchele kutoka Tandale, Tandika, Temeke, na Mbagala ambayo uhudumia masoko ya Mkuranga, Rufiji na Kilwa.
Wadau wengine waliohudhuria ni Mbeya Rice, KTC Kilombero Rice, MTC Morogoro wakiwakilisha vikundi vya wachakataji na wadau wa mchele wa Igawa na Ubaruku.
Akifungua semina hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Dennis Mwila aliwasisitiza wasindikaji na wafanyabiashara wa mchele kujipanga kimkakati katika kuhudumia na kuchangamkia fursa za masoko ndani na nje badala ya kutulia na kulalamika kukosa soko.
Naye, Mtaalamu kutoka TanTrade, Deo Shayo alibainisha maeneo ambayo mchele na nafaka za Tanzania kwa ujumla zinafanya vizuri kuwa ni katika Masoko ya Miji ya kibiashara ikiwemo Dar es Salaam na Arusha.
Alisema kwa upande wa masoko ya nje yanayoonekana kufanya vizuri zaidi katika zao hilo la mchele ni Kenya, Burundi, Uganda, Congo DRC, Zambia na Rwanda.
Aidha Shayo ametoa ushauri kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa mpya zinazoibuka za Biashara katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) ambapo wigo wa kuhudumia ni mkubwa kwenye nchi zaidi ya 50 kwa unafuu wa kodi ya forodha na pia walaji wengi.
“Pia wafanyabiashara mnatakiwa kushiriki matukio ya ukuzaji Biashara ya TanTrade ikiwemo Maonesho ya Sabasaba 28 Juni hadi 13 Julai 2023 ili kujitangaza zaidi,” alisema Shayo
Kwa upande wa Balaza la Mchele (RCT) limeahidi kuendelea kuwasaidia wazalishaji wa mchele katika masuala ya kushauri sera rafiki kwa kushirikiana na serikali ili kuimarisha uzalishaji na biashara za mchele nchini.
Kwa niaba ya wafanyabiashara waliopatiwa mafunzo hayo, Geofrey Rwiza na Leoncia Salakana wameishukuru RCT na Serikali kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuinua zaidi biashara za mchele kwani zimeajiri watu wengi na pia kuongoza katika mauzo ya nje hivi karibuni.
Hivyo wameomba matatizo yao ya mara kwa mara ikiwemo tozo wanapovuka halmashauri moja hadi nyingine zipunguzwe au kuondolewa kabisa ili kurahisisha ufanyaji wa biashara nchini.
Lengo la semina hiyo lilikuwa kutoa uelewa kuhusu biashara za mchele katika soko la ndani na kuwaunganisha wasindikaji na wadau wa masoko yenye walaji wengi ikiwemo Dar es Salaam ili waweze kuwa na mahusiano ya kibiashara na kutengeneza biashara endelevu.
Mpango huu wa mafunzo na kukutanisha wadau ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Baraza la Mchele Tanzania kwa kushirikiana na wafadhili na Mamlaka za Serikali ili kuboresha mnyororo wa thamani wa mpunga na bidhaa zinazohusiana.