NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SAMPULI kutoka zaidi ya watu 700 zimechukuliwa kwa ajili ya utafiti wenye lengo la kubaini kiini cha ongezeko la saratani kwa wakazi waishio mikoa ya Kanda ya Ziwa, Bunge limefahamishwa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, ufafiti huo upo katika hatua ya maabara ambapo wataalam wanafanya uchambuzi wa katika ngazi ya kimaumbile (Genetics).
Dk Mollel amelazimika kutoa maelezo hayo Bungeni Dodoma leo, Jumatano (Mei 15, 2023) wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge Neema Lugangira aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa katika utafiti huo.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri amesema hatua hizo zinafanywa kwa lengo la kubaini kiini cha tatizo katika mikoa hiyo iliyopo Kanda ya Ziwa.
Wakati huohuo, Wizara imesema kuwa iwapo mtu akiibuka na kujitangaza kuwa ana uwezo wa kutibu saratani, Wizara hutuma wataalam kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu pamoja Taasisi ya Tiba Asili kwa lengo la kuhakikisha kama kuna ukweli.
“Tunapogundua si kweli tunamzuia kufanya hivyo na kumtia moyo aendelee kufanya utafiti zaidi kwa kushirikiana na sisi,” Naibu Waziri alisema wakati akijibu swali la Mbunge Fatuma Tawfiq, aliyetaka kujua kauli ya Wizara juu ya waganga hao.