NA MWANDISHI WETU, DODOMA
NAIBU Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel ameeleza kuwa ukiwa na barua kutoka kwa mtendaji wako wa kata, unaweza kupata msamaha wa gharama za usafishaji wa figo.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Mollel amesema bungeni, Dodoma leo Jumatano (Mei 15, 2023).
Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Sabu alihoji maswali ya nyongeza akitaka kujua mambo ya kuzingatia ili mtu wa kipato cha chini aweze kupata msamaha wa matibabu hayo.
Aidha, alitaka kujua mpango wa Serikali wa kupunguza gharama za usafisaji figo [dialysis] kwa maelezo kuwa ni gharama kubwa kwa watu wenye kipato kidogo.
Akizungumzia juu ya utaratibu, Dk Mollel amesema endapo mtu akiwa na waraka huo kutoka ngazi ya kata, basi utaratibu wa msamaha unafanyika.
Awali, Naibu Waziri aliwaeleza wabunge kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali za rufaa za kanda na mikoa pamoja na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma.