NA MWANDISHI WETU, DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan amebainisha faida mbalimbali za kusogeza huduma za mawasiliano kwa wananchi wa vijijini ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za matibabu ya kimtandao.
Rais Samia ameeleza hayo leo Mei 13, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa minara ya simu vijijini kati ya serikali na watoa huduma ambao ni kampuni za Airtel Tanzania, TTCL, Vodacom Tanzania, Mic Tanzania (Tigo) na Viettel (Halotel).
Amesema huduma hizi za mawasiliano zinakwenda kuimarisha huduma za matibabu kimtandao vijijini, hivyo itarahisisha utoaji wa huduma hizo kwa wananchi wa pembezoni.
“Huduma hizi za mtandao zinakwenda kutusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Mradi mkubwa wa M-Mama ambao tuliuanza Tanzania na sasa unaibwa na wengine, tumekwenda kupunguza vifo hivi,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kwamba mifumo ya mawasiliano ikikaa vizuri kuanzia ngazi ya juu wizarani hadi kwenye vituo vya afya, inakwenda kuongeza usimamizi mzuri wa matumizi ya dawa na vifaa tiba katika vituo hivyo.
Rais Samia ameangazia pia suala la usalama akisema mawasiliano mazuri vijijini yatachochea na kukuza usalama wa nchi kwa watu kutoa taarifa za vitendo vinavyotishia usalama katika maeneo yao.
“Tunakwenda kukuza usalama ndani ya nchi yetu, ndani ya maeneo yetu kwa sababu lolote litakalotokea ni rahisi kufanya mawasiliano na hali za uharibifu wa usalama zinachukuliwa hatua,” amesema.
Mkuu huyo wa nchi amebainisha kwamba mradi huo wa mawasiliano vijijini utaiwezesha Serikali kutekeleza malengo endelevu ya maendeleo (SDGs) kama yalivyowekwa ikiwemo kupunguza hali ya kutokuwa sawa.
“Kuna lengo la 16 ambalo linazungumzia jinsi ya kutumia huduma na kuongeza uzalishaji. Hili nalo tunatekeleza, tunapopeleka huduma vijijini, wananchi wa huko wanatumia mitandao zaidi na kuongeza uzalishaji,” amesema kiongozi huyo.
Rais Samia amesisitiza kwamba wanakwenda kuongeza matumizi ya mitandao kwa huduma za kifedha kwa maeneo ya vijijini hasa yale ambayo hayakuwa na mtandao, jambo ambalo amesema litachochea shughuli za kiuchumi.
“Tunachokifanya leo kinakwenda kugusa sekta mbalimbali za nchi yetu, kinakwenda kugusa maendeleo mijini na vijijini ili watu tuende kwa kasi katika maendeleo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amemtaka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kupeleka suala la mawasiliano na Tehama kwa wadau ili watoa maoni yao jinsi wangependa kuona mitaala inakuwa.
“Sasa hivi kuna semina ya elimu inaendelea, tunataka wananchi watoe maoni kuhusu mitaala yetu. Nenda kalipeleke hili huko tupate pia maoni ya wananchi na nadhani mtashirikiana kabla semina haijaisha.
“Niwaombe wananchi watoe maoni wanavyoona tunaweza kwenda vizuri na mitaala yetu ya elimu. Tehama hii inakwenda kukuza elimu yetu kwa watoto wetu,” ameeleza Rais Samia wakati wa hotuba yake.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema walitangaza zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo 763 lakini baada ya mchakato wa zabuni, wamepata maeneo katika kata 713 ambayo minara ya mawasiliano 758 itakwenda kujengwa.
“Hii ni historia kwa taasisi yetu, hata ushiriki wa watoa huduma katika zabuni hii, wameweza kushiriki kwa asilimia 93. Hii ni historia katika ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali,” amesema Mashiba.
Mtendaji huyo amesema baada ya kutangaza zabuni hiyo, wamepata watoa huduma watakaokwenda kujenga minara ambao ni TTCL wanaokwenda kujenga minara 104 katika kata 104, Vodacom Tanzania ameshinda kata 190 ambapo atakwenda kujenga minara 190.
Wengine ni Airtel Tanzania ambayo imepata kata 161 ambapo itajenga minara 168, Tigo (MIC Tanzania) imeshinda katika maeneo 244 ambapo itajenga minara 262, Halotel (Vietel) imeshinda katika kata 34 na itakwenda kujenga minara 34 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mbali na kwenda kujenga minara, tunakwqenda pia kuongeza nguvu ya minara mingine 304 ambayo ilikuwa inatoa teknolojia ya 2G lakini sasa itakwenda kutoa teknolojia ya 3G na baadhi ya maeneo mengine itatoa teknolojia ya 4G,” amesema mtendaji huyo.
Ameongeza kwamba Tigo itakwenda kuongeza nguvu ya minara 148, TTCL minara 55, Airtel minara 32, Vidacom minara 69 na jumla itakuwa minara 304.